Friday, 26 January 2018

HADITHI SEHEMU YA NANE

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 08


Biashara ilimwendea vizuri, japokuwa hakuwa bosi lakini kwa kiasi fulani kila kitu kilikwenda kama alivyokuwa akitaka. Yeye ndiye alikuwa msafirishaji mkuu wa madawa hayo kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aliaminika mno kwa kuwa kila mzigo aliokuwa akitumwa ulifika salama mikononi mwa mtu aliyekuwa akihitajika kuupata mzigo huo. Siku zikaendelea kukatika, akaanza kuwa na maendeleo makubwa lakini tatizo lilikuja pale alipoanza kufanya starehe.
Kiasi kikubwa cha fedha alichokuwa akikipata kutoka katika biashara zile, alikiweka katika mstari wa starehe zake. Kila siku Ethan alikuwa mtu wa kubadilisha wanawake na kubadilisha viwanja kiasi kwamba kiasi cha fedha alichokuwa akikipata wakati mwingine hakikutosha kabisa.
Alisahau alipotoka, alisahau kama kule Manhattan alipokuwa kulikuwa na rundo la watoto masikini, watu wasiojiweza ambao kila siku maisha yao yalikuwa pembeni ya mapipa ya takataka. Alisahau kila kitu, aalichokuwa akikifanya kwa wakati huo kilikuwa ni starehe tu.
Wanawake walimopapatikia kwa kuwa hakuwa mchoyo, alichokuwa akikipata aligawana nao na hivyo kutengeneza jina kubwa masikioni mwao. Siku zikakatika na kukatika mpaka pale aliposikia taarifa kwamba bosi wake aliyekuwa akimuweka mjini, bwana Sanchez alikuwa hoi kitandani.
Kilichomlaza kilikuwa ni saratani ya damu, alikuwa akiugua kila siku kwa kutokwa na damu puani na mdomoni. Ugonjwa huo ulimuanza kwa kasi hali ambayo ilimfanya kupelekwa hospitali ambapo madaktari wakawaambia ndugu zake kwamba asingeweza kupona.
“Hawezi kupona ugonjwa huu, ni lazima afe,” alisema daktari, aliamua kuwaambia ukweli kwamba mgonjwa waliyekuwa wamempeleka ilikuwa lazima afe.
“Hawezi kupona?”
“Hawezi. Ni lazima afe.”
Kansa yake ilisababishwa na ubwiaji mkubwa wa madawa ya kulevya, hakuwa na nafuu hata kidogo walichokifanya ndugu zake ni kumchukua na kumrudisha nyumbani kumuuguza katika kipindi cha mwisho.
Walipomfikisha huko, wakamfungia chumbani kwake. Hawakutaka kumuacha hata kidogo na hawakutaka kumficha juu ya kile alichokisema daktari kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kufa hivyo kama alitaka kufanya vitu vyake kwa mara ya mwisho, alitakiwa kufanya kwa wakati huo.
“Nitagawa utajiri kwa watoto wangu! Niitieni mwanasheria wangu,” alisema bwana Sanchez.
Mwanasheria wake akaitwa na kisha kuandika kile alichotakiwa kuandika, mirathi ikagaiwa kwa watoto wote. Kitu ambacho hakukiamini Ethan ni kwamba hakukuwa na mali yoyote aliyoachiwa japokuwa yeye alikuwa mtu wa karibu sana na mzee huyo.
Bwana Sanchez alipofariki hapo ndipo maisha yalipomgeukia, akaanza kurudi kule alipotoka, bisahara zikakata, mitego yote aliyokuwa ametega ikaharibika vibaya, marafiki zae ambao kila siku alifanya nao starehe wakamkimbia kwani waliona kwamba hakuwa na kitu tena.
Aliogopa kurudi New York katika mtaa aliozaliwa kwa kuhisi kwamba bado alikuwa akitafutwa sana, hivyo alichokifanya ni kukimbilia Texas, sehemu iliyokuwa na mpaka mkubwa wa kuingilia nchini Mexico.
Huku akiwa huko ndipo alipokumbuka kwamba mara ya mwisho alikutana na mzee mmoja ndani ya ndege ambaye alimwambia sana kuhusu biashara ile ya madawa kwamba haikuwa nzuri hivyo alitakiwa kuachana nayo.
“Namba yake niliiweka wapi?” alijiuliza.
Hicho ndicho kilichomuumiza kichwa wakati huo, hakukumbuka mahali alipoihifadhi namba ile, alikumbuka vilivyo kwamba alipewa na kurudi nayo nyumbani, baada ya hapo, hakukumbuka aliiweka wapi kwani kilipita kipindi kirefu mno na hata kumbukumbu zake zikawa zimepotea kabisa.
“Nilirudi nyumbani nikiwa nacho, nikakaa kitandani, baada ya pale nilikiweka wapi? Mhh! Hapana! Mbona sikumbuki vizuri?” alijiuliza lakini akakosa jibu.
Aliendelea kupigika mitaani, maisha yakampiga sana. Alipoona kwamba kila kitu kinakwenda kombo hapo ndipo alipoingia katika biashara ya kuuza magari, yaani walikuwa wakiiba magari nchini Marekani, wanayapitisha kwa njia za panya kuelekea Mexico na kuyauza huko.
Hakuwa na jinsi, japokuwa ilikuwa ni kazi ya hatari iliyohatarisha maisha yake lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kupambana ili atoke katika umasikini mkubwa uliompigia hodi mlangoni. 
“Ushawahi kuiba Lambonghin?”
“Hapana!”
“Sasa leo tunakwenda kuiiba, kama tukifanikiwa, sisi matajiri,” alisema jamaa yake, walikuwa wezi wakubwa hapo Texas.
“Hakuna noma, ila hatuwezi kukamatwa?”
“Tutakamatwa vipi? Kama tumewahi kuiba magari zaidi ya mia tano, tutakamatwaje kwa gari moja?” aliuliza rafiki yake huyo.
“Basi sawa. Lipo wapi?”
Huo ndiyo mpango waliopanga siku hiyo, walitaka kuiba gari ya thamani na kisha kuisafirisha kwa njia za panya mpaka nchini Mexico. Kuhusu kuiba, hilo wala halikuwa tatizo kabisa, waliweza kufanya hivyo ila kazi kubwa waliyokuwa nayo mahali hapo ni kulitoa gari hilo sehemu lilipokuwa na kulipeleka huko walipotaka kulipeleka.
Saa mbili usiku wakakutana karibu kabisa na ukumbi mmoja wa starehe, mbele yao kulikuwa na magari mengi lakini miongoni mwa magari hayo, kulikuwa na gari moja la thamani sana lililokuwa na gharama zaidi ya dola mioni tano, zaidi ya bilioni moja, ilikuwa lambonghin nyekundu iliyoonekana kuwa mpya kabisa.
Walikuwa wazoefu wa kuiba magari, hata kuiba gari hilo wala haikuwasumbua kabisa. Kwa sababu Ethan alikuwa mtaalamu mkubwa wa kuendesha magari, akakaa sehemu ya dereva, kwa kutumia utundu kwa kuunganisha nyaya, wakaunganisha na gari kuwaka, kilichobakia ni sauti za watu huko nyuma.
Hapo ndipo walipoanza safari ya kuelekea mpakani kwa njia za panya ili waweze kuliingiza gari hilo nchini Mexico. Walipanga kwamba huo ndiyo ungekuwa wizi wao wa mwisho hivyo baada ya hapo wangeacha kabisa kwani ilikuwa moja ya kazi ya hatari kabisa kuwahi kuifanya.
“Hivi unakanyaga mafuta kweli?” 
“Ndiyo!”
“Upo ngapi hapo?”
“180 kwa saa!”
“Gari mwisho ngapi?”
“400 kwa saa!”
“Sasa hizo nyingine unamuachia nani?”
“Ebwana tutakufa.”
“Kama kufa acha tufe, kuna raha gani ya kuishi, kama kufa tutakufa hata ukiendesha 1 kwa saa, kanyaga moto kaka,” alisema rafiki yake.
Mwendo aliokuwa akiendesha ulikuwa ni wa kasi mno, gari lilikuwa likijiweza kwa kasi hivyo Ethan hakuwa na jinsi, akaanza kukanyaga mafuta mpaka kuhisi kwamba gari hilo lingeweza kupaa. 
Kutokana na kuwa usiku mwingi, barabarani hakukuwa na magari kabisa, walitembea kwa mwendo waliotaka tena kwa kasi zaidi na baada ya masaa mawili walitaraji kufika karibu na mpaka huo ambapo wangechukua njia za panya na kuingia Mexico.
Wakati wamebakiza kilometa tatu kabla ya kuingia katika kituo cha mafuta cha Gapco, kwa mbali wakaanza kuyaona magari ya polisi yakiwa yamesimama barabarani huku taa zikiwaka.
Kwanza wakaogopa, kwa kasi waliyokuwa wakienda nayo walijua kwamba endapo wangeyagonga magari yale basi ingekuwa kifo chao hivyo alichokifanya Ethan ni  kupunguza kasi na kisha kuchukua barabara nyingine ya vumbi, magari yale ya polisi yakawashwa na kanza kuwafuata.
“Kanyaga mafuta!”
“Haiwezekani! Hakuna lami huku,” alisema Ethan.
Walikwenda na gari hilo kwa umbali mrefu mpaka mafuta yalipowaishia. Hawakuwa na jinsi, wasingeweza kubaki na wakati polisi waliendelea kuwasogelea kule walipokuwa, walichokifanya ni kuteremka na kisha kuanza kukimbia huku wakiwa wamelitelekeza gari lile.
Walikimbia kwa umbali mrefu, mbele kabisa wakakutana na korongo kubwa, lilionyesha kwamba mchana huwa kunakuwa na watu wanaochimba kokoto kutokana na ardhi ya Texas kuwa na kokoto nyingi, walichokifanya ni kuingia katika korongo lile na kuendelea na safari yao.
Hawakutaka kusimama sehemu yoyote ile, walichokuwa wakikitaka ni kufika walipotaka kufika pasipo kugundua kwamba polisi wale wa nyuma walipoona wezi wale kule walipokimbilia, wakawasiliana na polisi wa mpakani na kuwapa taarifa, nao wakaanza kusogea kule walipoambiwa wezi wale walipokimbilia, kwa maana hiyo, kadiri Ethan na rafiki yale walivyokuwa wakipiga hatua, ilikuwa ni sawa na kuwasogelea polisi hao waliotoka mpakani.


INAENDELEA...

No comments:

Post a Comment