BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 06
Maisha yaliendelea
kama kawaida. Hakukuwa na kitu kilichokisumbua kichwa cha padri Benedicto kama
kumuona mzazi mwenzake akiishi mbali naye. Hakuwa na uwezo wa kwenda kukaa naye
lakini kila siku alikuwa mtu wa kutamani kumuona mwanamke huyo akiwa karibu
naye kwani ndiye mtu pekee aliyeonekana kuwa faraja katika maisha yake.
Kutokana na mapenzi
mazito aliyokuwa nayo juu yake, muda wote alihisi kwamba alikuwa akiibiwa tu.
Aliwafahamu vijana wa Sinza, walikuwa vijana makini kuhusu masuala yote ya
mapenzi, walikuwa na uwezo mkubwa wa kumteka msichana yeyote hata kama angekuwa
mgumu kiasi gani.
Hakutaka kusalitiwa,
alitaka Irakoze awe wake peke yake, hivyo alichokifanya ni kuanza kupanga
mipango kabambe ya kumbana mwanamke huyo kwa kumpeleka katika Chuo cha Utawa,
St. Mary’s Catholic kilichokuwa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam na
kuingia pale kama mpishi.
Mipango yote ya
Irakoze kuingia ndani ya chuo kile ilifanywa na padri Benedicto huku akimchukua
Annabel na kumpeleka nchini Marekani kwa ajili ya kusoma huko katika Shule ya
Consolatha Seminary School iliyokuwa katika Jiji la New York nchini Marekani.
Kidogo moyo wake
ukawa na amani, kutokana na umbo lake kuwa dogo na sura ya kitoto aliyokuwa
nayo, mara baada ya kufika katika chuo hicho cha Utawa, masista wote walihisi
kwamba Irakoze alikuwa msichana mdogo, hivyo wakamchukulia hivyohivyo.
Kila siku alikuwa
hapo huku akiwasiliana na padri Benedicto simuni, bado wawili hao waliendelea
kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa siri sana kiasi kwamba hakukuwa na mtu
yeyote aliyefahamu kilichokuwa kikiendelea.
Huo ulikuwa mwaka
wake wa kwanza chuoni hapo, alionekana kuwa mtu mwenye heshima, alimheshimu
kila mtu kuanzia wale wa chini mpaka wa juu. Wasichana wengi waliokuwa chuoni
hapo walimpenda Irakoze ambaye walipenda kumuita kwa jina la Sista Magdalena.
Siku zikaendelea
kukatika, kila alipokuwa akitumwa mjini kwa ajili ya kununua baadhi ya vitu kwa
ajili ya shule hiyo, alikuwa akienda na kuonana na padri Benedicto na kisha
kulala wote hata kwa masaa mawili kisha kurudi chuoni.
Huko ndipo alipopata
taarifa kuhusu binti yake aliyekuwa nchini Marekani. Masomo yaliendelea vizuri
na mara kwa mara safari za Benedicto kuelekea nchini Marekani hazikuisha, kila
alipokwenda, alihakikisha anaonana na binti yake na kisha kurudi nchini
Tanzania.
“Amekua sana, mwaka
wa sita huu,” alisema Benedicto, alikuwa akimwambia Irakoze.
“Nina kiu ya
kumuona.”
“Usijali! Ila nataka
tuifanye kitu kimoja”
“Kipi?”
“Na wewe usomee
utawa!”
“Mmmh!”
“Hakuna tatizo!
Utafanikiwa tu, nataka uwe na safari za kutosha kwenda Ulaya na sehemu
nyingine,” alisema Benedicto.
“Sawa! Hakuna
tatizo!”
Hilo ndilo walilokuwa
wamekubaliana, ilikuwa ni lazima Irakoze aanze kusomea utawa ndani ya chuo
hicho alichokuwa akifanya kazi kama mpishi. Hilo wala halikuwa tatizo, kwa
sababu tayari alikwishafanya kazi hiyo kwa miaka mitatu, akachukuliwa na kuanza
masomo moja kwa moja.
Kila siku alikuwa
akiamka asubuhi na mapema kama wanachuo wengine na kisha kuelekea kanisani
ambapo walisali kisha kujiandaa na masomo kama kawaida. Japokuwa hakuwa amesoma
sana kipindi cha nyuma lakini uwezo wake wa kawaida ulitosha kabisa kuonyesha
kwamba kama angeendelea zaidi basi angeweza kufanikiwa sana katika maisha yake.
Aliishi kama mtumishi
wa Mungu, kila wakati alikuwa mtu wa kusali huku rozali ikiwa shingoni mwake.
Kila mtu alimheshimu na alipoonekana kwamba yeye ndiye alikuwa mcha Mungu
mkubwa kuliko wengine, wakampa uongozi wa bweni pasipo kujua kwamba mwanamke
huyo alikuwa na mtoto ambaye alikuwa akisoma nchini Marekani.
Padri Benedicto
hakuacha, kwa kuwa katika kila hatua aliyokuwa akipitia Irakoze ilikuwa chini
yake, hivyo alihakikisha kwamba hata kwenda nje ya chuo hicho linakuwa jambo
jepesi ili mradi mwisho wa siku aweze kuonana naye na kufanya mambo yao.
Alichokifanya ni
kukaa chumbani na kuandika barua, alikuwa akiuandikia uongozi wa chuo hicho
kwamba kutokana na heshima aliyokuwa nayo Irakoze, aliruhusiwa kila Jumapili
kwenda kusali nje ya chuo hicho.
Nafasi hiyo
haikutolewa mara kwa mara, ilitolewa mara chache sana tena kwa wanachuo
walioonekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Kwa Irakoze hakukuwa na mtu
aliyeonekana kuwa na wasiwasi, jinsi nidhamu yake ilivyokuwa chuoni hapo,
ilimfanya kila mmoja kukubaliana na padri Benedicto kutokana na jinsi
alivyokuwa chuoni hapo.
Hiyo ndiyo ilikuwa
nafasi nyingine na waliitumia vilivyo kuwa pamoja. Kila kitu kilichokuwa
kikifanyika kiliendelea kuwa siri kubwa. Baada ya miaka miwili kukatika,
hatimaye aliyekuwa Kardinari wa Kanisa la Kiroma nchini Tanzania, Paulo Alonso
akafariki dunia na hatimaye barua kuandikwa kutoka Vatican kwamba Padri
Benedicto alitakiwa kutawazwa na kuchukua nafasi hiyo kwani kwa sifa zote za
kuwa kardinari alikuwa nazo.
“Lakini kwa nini
apewe padri? Kwa nini asipewe askofu?” maaskofu waliulizana tu.
“Hata sisi
hatufahamu, ila kwa sababu ni barua iliyoletwa kutoka Vatican, hatuna budi,
acha tukubaliane nayo,” alisema askofu mmoja.
Baada ya wiki mbili,
padri Benedicto alitakiwa kuelekea nchini Vatican kwa ajili ya kutawazwa na
hatimaye kuwa kardinari mkubwa nchini Tanzania. Hiyo ilikuwa nafasi yake pekee,
moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, hakukuwa na kitu kilichowahi kumpa furaha
maishani mwake kama kipindi hicho.
Suala la kuwa na
mtoto liliendelea kuwa siri yake, hakutaka mtu yeyote afahamu na alikuwa
akijitahidi kufanya kila liwezekanalo kusiwe na mtu yeyote anayelifahamu hilo.
Kwenye kila mwaka, alikuwa akimtumia mtoto wake Annabel kiasi cha fedha kwa
kutumia akaunti nyingine kabisa iliyosomeka kwa jina la Andrew McDonald, raia
kutoka nchini Kenya.
Japokuwa Annabel
katika kipindi hicho alikuwa na miaka kumi, lakini aliendelea kufichwa kwamba
baba yake alikuwa padri ambaye katika kipindi hicho alitarajiwa kutawazwa na
kuwa kardinari nchini Tanzania.
“Unataka kuwa nani
ukikua?” aliuliza Benedicto.
“Nataka kuwa
mwanasheria.”
“Kwa nini usiwe
sista?”
“Sitaki! Nitataka
niolewe. Nimesikia kwamba sista haolewi! Kweli baba?”
“Ndiyo!”
“Basi mimi nataka
kuwa mwanasheria, ninataka kuolewa baadaye!”
Alikuwa akizungumza
na binti yake katika kipindi alichokwenda kumtembelea nchini Marekani. Japokuwa
alikuwa nchi nyingine lakini kofia aliyokuwa ameivaa haikutoka kichwani mwake.
Shule hiyo aliyompeleka binti yake kusoma ilimtunza vizuri, alipata malezi yote
na hakukuwa na shida sana kwa kuwa mara kwa mara alikuwa akifika hapo na
kumuona.
Annabel alikuwa binti
mzuri, mwenye sifa zote za kuitwa mrembo. Alichanganyikana, alikuwa na sura ya
baba yake lakini pia alikuwa na sura ya mama yake. Watu wengi waliokuwa
wakimuona, walikiri kwamba binti huyo angekuja kutikisa sana siku za usoni
kutokana na urembo wake huo.
“Baba!”
“Naam!”
“Unafanya kazi gani?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Kwani sijawahi
kukwambia binti yangu?”
“Hapana!
Hukuniambia!”
“Mimi ni
mfanyabiashara binti yangu, huwa nasafirisafiri sana,” alijibu Benedicto.
“Kweli baba?”
“Ndiyo! Nikitoka
hapa, nakwenda Dubai, nikuletee zawazi gani nikija?”
“Chochote upendacho
baba, nitafurahi!” alisema Annabel.
Benedicto hakuwa na
jinsi, ni kweli alimpenda binti yake lakini kulikuwa na vitu ambavyo hakutakiwa
kuwa mkweli kabisa, alimdanganya kwamba alikuwa mfanyabishara kwa kuwa hakutaka
ajue kwamba alikuwa padri ambaye hakutakiwa kuoa au kuwa na mtoto yeyote yule.
Kwake, bado lile
liliendelea kuwa siri kubwa, kila siku lilimuumiza moyoni mwake lakini hakuwa
na jinsi, alikubaliana na kila kitu kilichokuwa kiiendelea, na hata kama
alifanya dhambi, aliamini kwamba hakukuwa na mwanadamu aliyekuwa mkamilifu
mbele za Mungu.
Baada ya siku tatu,
akarudi nchini Tanzania ambapo moja kwa moja akawasiliana na Irakoze na
kumwambia kuhusu mtoto wao na ndoto aliyotaka kuwa nayo katika maisha yake.
“Kakataa kuwa sista?”
“Amekataa!”
“Daaah! Ngoja niende,
nitazungumza naye,” alisema Irakoze.
“Hakuna tatizo!”
Japokuwa aliamini
kwamba binti yake angeweza kumsikiliza na hatimaye kukubaliana nao kuwa sista
lakini hilo halikuwezekana, bado msimamo wa Annabel ulikuwa ni kuwa mwanasheria
mkubwa duniani.
Hakukuwa na mtu
aliyemzuia, waliachana naye, aendelee na maisha yake na mwisho wa siku
kukamilisha kile alichokuwa akikitaka.
Wakati Annabel
akifikisha miaka kumi na sita, alionekana kuwa binti mrembo mno, kipindi kirefu
cha maisha yake alikitumia nchini Marekani, hakuwahi kurudi nchini Tanzania,
aliondoka huko miaka mingi iliyopita, tangu alipokuwa na miaka minne.
Hakufahamu sehemu
yoyote nchini Tanzania, hakufahamu mitaa na hata watu wa huko walikuwa na
utamaduni gani. Baada ya kufikisha miaka hiyo, hakutaka kukaa nchini Marekani,
alitaka kuwa na muda wa kurudi nchini Tanzania ili aweze kukaa na wazazi wake
ambao hakuwahi kukaa nao hata siku moja.
Alitaka malezi yao,
alichokifanya ni kuwasiliana nao, hawakuwa najinsi, wakajipanga kwamba mara
binti yao atakapofika nchini Tanzania, wampelekea katika nyumba yao nyingine
iliyokuwa Kisarawe, pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo waliamini kwamba
hakukuwa na watu wengi.
Siku ya safari
ilipofika, Annabel akaingia ndani ya ndege tayari kwa kurudi nchini Tanzania.
Hapo Marekani akapanda ndege ya Shirika la Ndege la American Airlines ambayo
ilikuwa ikifanya safari mpaka nchini Uingereza, Italia na baadaye kuelekea
Uholanzi ambapo huko wangebadilisha ndege na kuelekea Dubai, kisha India na
Kenya jijini Nairobi na kuingia nchini Tanzania kabla ya kuelekea Afrika
Kusini.
Baada ya abiria
kutakiwa kuingia ndani ya ndege hiyo, Annabel akasimama na kuanza kuelekea
ndani ya ndege hiyo. Kwa muonekano, alionekana kuwa binti mkubwa, mrembo,
mwenye mvuto ambaye alivutia sana, kila mwanaume aliyemwangalia, alitamani kuwa
na msichana mrembo kama alivyokuwa.
Wakati ameingia ndani
ya ndege hiyo na kukaa katika viti vya watu wawili, akaja mwanaume mmoja,
alionekana kuwa kijana mtanashati, aliyependeza, alivalia suti ya gharama, muda
wote uso wake ulionekana kuwa na tabasamu pana, alimuona Annabel, tabasamu
likaongezeka usoni mwake.
“How are you cute,”
(Habari yako, mrembo) alimsalimia Annabel.
“I’m fine, you are
welcome,” (Salama, karibu) alimkaribisha mwanaume yule aliyejitambulisha kwa
jina la Ethan Dylan.
No comments:
Post a Comment