Sunday, 28 January 2018

HADITHI!!!!!!!!!!................. SEHEMU YA KUMI

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 10


Ni kweli walishtuka, hawakuamini kile walichokisikia kwamba mbali na kuwatafuta wanawake waliotakiwa kuwapeleka kwa ajili ya kuigiza filamu, kulikuwa na kazi nyingine ya ziada ambayo iliitwa Biashara ya Kifo.

“Ndiyo inakuwaje hiyo?”

“Ni kazi rahisi tu japokuwa unahitajika umakini wa hali ya juu,” alisema bwana Cook.

Hapo ndipo mzee huyo alipoanza kueleza namna ambavyo biashara hiyo ilitakiwa kufanyika. Kulikuwa na kundi la wanawake mitaani waliokuwa wakihitaji ajira, watu waliokuwa wakitafuta ajira kila siku, mbali na hiyo, kulikuwa na kundi kubwa la wanawake ambao kila siku walitamani kufika nchini Marekani.

Hao ndiyo waliotakiwa kufanyiwa biashara hii. Kazi ilikuwa ni kuwafuata na kuanza kuwalaghai kwa maneno matamu kwa kuwaahidi kwamba wangewapa ajira yenye kiasi kikubwa cha fedha na hivyo wawasafirishe kwenda nchini Marekani, wanapofika huko, walazimshwe kuigiza filamu za ngono, kwa atakayetaka kuendelea basi aendelee lakini kwa wale ambao wangekataa kuendelea na kulilia kurudi nyumbani, basi hao wauawe na kisha kuchunwa ngozi ambayo ingepelekwa nchini China kwa ajili ya kutengenezea vitu vya asili.

“Mmmh!” aliguna Ethan.

“Unahisi ni kazi ngumu?”
“Kwangu! Kuchuna ngozi ya binadamu, sijawahi kufanya kazi hiyo,” alijibu Ethan.

“Kazi yako si kuchuna ngozi, kazi yako kubwa ni kutafuta wasichana tu, hakuna jingine, hiyo ni kazi ya watu wengine,” alisema bwana Cook.

“Kama ndiyo hivyo, hakuna shida.”

Hiyo ndiyo kazi aliyoahidiwa kulipwa kiasi kikubwa cha fedha. Kilichofanyika ni kupewa kiasi cha dola elfu hamsini ambazo zilikuwa ni zaidi ya milioni hamsini, akatengenezewa pasipoti kubwa kwa ajili ya kusafiria nchi hadi nchi na kisha kuanza safari za kuwatafuta wasichana kwa ajili ya kuigiza filamu za ngono.

Safari yao ya kwanza kabisa kwenda ilikuwa nchini Hispania, huko wakakutana na wasichana kadhaa na kuhitaji kufanya nao mahojiano kwa ajili ya kazi za uongo walizowaambia kwamba zilikuwa nyingi nchini Marekani.

“Upo tayari?”

“Kiasi gani?”

“Dola elfu moja kwa siku,” alijibu Ethan.

“Mmmh! Ni kazi gani?”
“Zipo nyingi tu lakini unatakiwa kuchagua. Kuna kazi za hotelini, kupika na nyingine nyingi,” alisema Ethan.

“Nipo tayari!”

“Sawa.”
“Si umesema Marekani?”
“Ndiyo!”

“Hakuna tatizo!”

Kutokana na wimbi kubwa la wasichana wa Ulaya kukosa ajira na kutamani sana kwenda nchini Marekani kwa kuamini kwamba kulikuwa na maisha mepesi, wakakubaliana na Ethan na mwisho wa siku kuelekea huko.

Ishu zote za usafirishaji zilikuwa chini yake, alitumia kiasi kikubwa cha fedha alichopewa na bwana Cook hivyo hakukuwa na tatizo lolote lile. Walipofika nchini Marekani katika Jiji la New York ambapo ndipo kulipokuwa makao makuu ya kampuni hiyo ya filamu za utupu, wakapelekwa hotelini na kuambiwa wasubiri.

“How many are they?” (Wapo wangapi?)

“Ten young girls!” (Wasichana wadogo kumi)

“What do you mean? Below 18?” (Unamaanisha nini? Chini ya miaka kumi na nane?) aliuliza bwana Cook.

“No! Above 18 but below 23,” (Hapana! Zaidi ya miaka 18 lakini chini ya miaka 23)

“Ok!” (Sawa)

Mara baada ya kufika katika hoteli hiyo, wakaambiwa waoge kwa ajili ya chakula cha usiku na siku inayofuata wangeanza safari ya kuelekea katika eneo la kazi, kule walipotakiwa kufanya kazi.

Kila mmoja alikuwa na furaha mno, kutoka nchini Hispania mpaka kufika nchini Marekani, tena kufanya kazi ndogo kwa mshahara mkubwa ilionekana kuwa kama bahati kwao. Sheria moja kubwa waliyokuwa wamepewa ni kutokutumia simu tu.

Waliufurahia usiku huo kwa kuona kwamba ndiyo ilikuwa mwanzo wa safari yao ya kuwa mamilionea mara watakaporudi nchini mwao, hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba nyuma ya pazia kulikuwa na zoezi zima la kuigiza filamu za utupu na kama kungekuwa na yeyote atakayekataa basi ilikuwa ni lazima auawe na kuchunwa ngozi.

“Andikisheni majina yenu na nafasi unazotaka kufanya kazi,” alisema Ethan, alikuwa akiwaambia wasichana hao kumi ambao wakafanya kama walivyotakiwa kufanya.

Siku iliyofuata Ethan akarudi hotelini hapo kisha kuwachukua, akawapeleka katika jumba moja kubwa lililokuwa pembezoni mwa Jiji la New York, aliwaandaa kwa ajili ya kazi aliyotaka kuwapa. Kwa kuwaangalia wasichana wale, walionekana kuwa na furaha kubwa kwa kuamini kwamba huo ungekuwa mwanzo tu kwani hata mapokezi waliyokuwa wamepewa siku hiyo yalikuwa makubwa na ya kifahari.
Wakateremka kutoka garini na kuingia ndani ya jumba moja kubwa, humo wakaambiwa watulie kwani kulikuwa na mtu aliyetaka kuzungumza nao. Wakatulia vitini na Ethan kuelekea chumbani. Baada ya dakika moja akarudi na mwanaume mmoja, alikuwa mtu mwenye umri mkubwa ambapo kwa kumwangalia tu, ungehisi kwamba alikuwa na miaka zaidi ya hamsini.

“Karibuni sana,” aliwakaribisha mzee huyo.

“Asante sana,” waliitikia kwa pamoja.

“Mpo hapa kwa ajili ya kufanya kazi, si ndiyo?”
“Ndiyo!”

“Kazi ipo, ila mmekwishaambiwa ni kazi gani mtakayofanya?”

“Hotelini!”

“Sawa! Ila kwa bahati baya huko kazi imekwisha, iliyobakia ni moja tu,” alisema mzee huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Gregory.

Wasichana wale walipoambiwa kwamba kazi ya hotelini ambao walikuwa wameifuata ilikwisha, kila mmoja akanyong’onyea lakini walipoambiwa kwamba kulikuwa na kazi nyingine ambayo ilikuwepo mahali hapo, wakarudi kwenye tumaini jipya.

“Kazi gani?”
“Mnajua kuigiza?”

“Mimi najua...” alisema msichana mmoja.

“Hata mimi najua,” alisema mwingine, mwisho kabisa, wote walisema wanajua.

“Nani anamjua Blue Diamond?”

“Mimi simfahamu.”

“Mimi namfahamu! Ni mcheza filamu za utupu,” alijibu msichana mmoja.

“Sawasawa! Blue alikuwa msichana kama nyie, wakati alipotoka nchini Canada, alifikia ndani ya nyumba hiihii, alikuwa masikini sana, lakini tukayabadilisha maisha yake na kuwa tajiri namna hiyo. Tulipomwambia kuhusu kuigiza filamu hizo, aliogopa sana lakini sasa hivi anatushukuru na kutulaumu kwa kuwa tulimchelewa kumwambia juu ya mafanikio makubwa ambayo angeyapata.

“Sasa hivi Blue ni msichana mwenye mafanikio, anaoglelea kwenye bwawa la fedha, anaendesha gari analotaka. Wangapi mpo tayari kuwa kama Blue?” alisema mzee Gregory na kumalizia na swali.

“Kuwa muigizaji wa filamu za utupu?” aliuliza msichana mmoja.

“Ndiyo! Hatukulazimishi kuigiza, hakuna mtu anayelazimishwa kuyafuata mafanikio na utajiri. Huwa tunalipa dola elfu tatu kwa kila kipande kimoja kwenye filamu zetu, kwa maana hiyo ikitokea ukafanya mapenzi na wanaume wawili kwa mpigo, utapata dola elfu sita,” alisema mzee huyo.

Kiasi cha fedha ambacho walitajiwa kilikuwa kikubwa mno zaidi ya milioni sita kwa mtu mmoja na milioni kumi na mbili kama utafanya mapenzi na wanaume wawili kwa pamoja, kila aliyekisikia, alitamani kukipata hapohapo lakini tatizo likawa namna ya kuigiza filamu hizo.  Wasichana hao wakaanza kutoa minong’ono ya chinichini lakini mzee yule aliendelea kuwaambia kwamba ilikuwa ni lazima wafikie mafanikio kama wangekubaliana nae.

Ili kuendelea kuwalaghai, wakawaletea mikataba na kuwawekea mbele yao, walitakiwa kusaini kisha kuandika akaunti zao ili mara watakapoanza kuigiza basi wawekewe kiasi hicho cha fedha.

“Mimi sipo tayari,” alisema msichana mmoja.

“Hata mimi sipo tayari,” alisema msichana mwingine.

“Sawa! Hakuna tatizo!”

“Mimi nipo tayari!”

“Safi sana!”

Kati ya wasichana kumi, wanne walikuwa tayari, wakakubaliana na mzee Gregory kisha kuambiwa wabaki mahali hapo huku wale sita waliokataa wakiambiwa warudi hotelini tayari kwa kujiandaa na safari siku ijayo kurudi nchini Hispania.


Wakasimama na kutolewa nje, wakaingizwa ndani ya gari huku Ethan akiwa pamoja nao. Gari halikwenda hotelini, lilibadilisha njia na kwenda katika jumba jingine kabisa, wao wenyewe walishangaa, hawakujua waliletwa pale kwa ajili gani, wakashushwa na kuingizwa ndani ya jumba lile, lengo kamili lilikuwa ni kuuawa na kisha kuchunwa ngozi, hiyo ndiyo ilikuwa Biashara ya Kifo, walitakiwa kuuawa na ngozi zao kutumwa nchini China ambapo kulikuwa na biashara nzuri tu.

No comments:

Post a Comment