BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 08
Biashara ilimwendea
vizuri, japokuwa hakuwa bosi lakini kwa kiasi fulani kila kitu kilikwenda kama
alivyokuwa akitaka. Yeye ndiye alikuwa msafirishaji mkuu wa madawa hayo kutoka
sehemu moja kwenda nyingine.
Aliaminika mno kwa
kuwa kila mzigo aliokuwa akitumwa ulifika salama mikononi mwa mtu aliyekuwa
akihitajika kuupata mzigo huo. Siku zikaendelea kukatika, akaanza kuwa na
maendeleo makubwa lakini tatizo lilikuja pale alipoanza kufanya starehe.
Kiasi kikubwa cha
fedha alichokuwa akikipata kutoka katika biashara zile, alikiweka katika mstari
wa starehe zake. Kila siku Ethan alikuwa mtu wa kubadilisha wanawake na
kubadilisha viwanja kiasi kwamba kiasi cha fedha alichokuwa akikipata wakati
mwingine hakikutosha kabisa.
Alisahau alipotoka,
alisahau kama kule Manhattan alipokuwa kulikuwa na rundo la watoto masikini,
watu wasiojiweza ambao kila siku maisha yao yalikuwa pembeni ya mapipa ya
takataka. Alisahau kila kitu, aalichokuwa akikifanya kwa wakati huo kilikuwa ni
starehe tu.
Wanawake
walimopapatikia kwa kuwa hakuwa mchoyo, alichokuwa akikipata aligawana nao na
hivyo kutengeneza jina kubwa masikioni mwao. Siku zikakatika na kukatika mpaka
pale aliposikia taarifa kwamba bosi wake aliyekuwa akimuweka mjini, bwana
Sanchez alikuwa hoi kitandani.
Kilichomlaza kilikuwa
ni saratani ya damu, alikuwa akiugua kila siku kwa kutokwa na damu puani na mdomoni.
Ugonjwa huo ulimuanza kwa kasi hali ambayo ilimfanya kupelekwa hospitali ambapo
madaktari wakawaambia ndugu zake kwamba asingeweza kupona.
“Hawezi kupona
ugonjwa huu, ni lazima afe,” alisema daktari, aliamua kuwaambia ukweli kwamba
mgonjwa waliyekuwa wamempeleka ilikuwa lazima afe.
“Hawezi kupona?”
“Hawezi. Ni lazima
afe.”
Kansa yake
ilisababishwa na ubwiaji mkubwa wa madawa ya kulevya, hakuwa na nafuu hata
kidogo walichokifanya ndugu zake ni kumchukua na kumrudisha nyumbani kumuuguza
katika kipindi cha mwisho.
Walipomfikisha huko,
wakamfungia chumbani kwake. Hawakutaka kumuacha hata kidogo na hawakutaka
kumficha juu ya kile alichokisema daktari kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima
kufa hivyo kama alitaka kufanya vitu vyake kwa mara ya mwisho, alitakiwa kufanya
kwa wakati huo.
“Nitagawa utajiri kwa
watoto wangu! Niitieni mwanasheria wangu,” alisema bwana Sanchez.
Mwanasheria wake
akaitwa na kisha kuandika kile alichotakiwa kuandika, mirathi ikagaiwa kwa
watoto wote. Kitu ambacho hakukiamini Ethan ni kwamba hakukuwa na mali yoyote
aliyoachiwa japokuwa yeye alikuwa mtu wa karibu sana na mzee huyo.
Bwana Sanchez
alipofariki hapo ndipo maisha yalipomgeukia, akaanza kurudi kule alipotoka,
bisahara zikakata, mitego yote aliyokuwa ametega ikaharibika vibaya, marafiki
zae ambao kila siku alifanya nao starehe wakamkimbia kwani waliona kwamba
hakuwa na kitu tena.
Aliogopa kurudi New
York katika mtaa aliozaliwa kwa kuhisi kwamba bado alikuwa akitafutwa sana,
hivyo alichokifanya ni kukimbilia Texas, sehemu iliyokuwa na mpaka mkubwa wa
kuingilia nchini Mexico.
Huku akiwa huko ndipo
alipokumbuka kwamba mara ya mwisho alikutana na mzee mmoja ndani ya ndege
ambaye alimwambia sana kuhusu biashara ile ya madawa kwamba haikuwa nzuri hivyo
alitakiwa kuachana nayo.
“Namba yake niliiweka
wapi?” alijiuliza.
Hicho ndicho
kilichomuumiza kichwa wakati huo, hakukumbuka mahali alipoihifadhi namba ile,
alikumbuka vilivyo kwamba alipewa na kurudi nayo nyumbani, baada ya hapo,
hakukumbuka aliiweka wapi kwani kilipita kipindi kirefu mno na hata kumbukumbu
zake zikawa zimepotea kabisa.
“Nilirudi nyumbani
nikiwa nacho, nikakaa kitandani, baada ya pale nilikiweka wapi? Mhh! Hapana!
Mbona sikumbuki vizuri?” alijiuliza lakini akakosa jibu.
Aliendelea kupigika
mitaani, maisha yakampiga sana. Alipoona kwamba kila kitu kinakwenda kombo hapo
ndipo alipoingia katika biashara ya kuuza magari, yaani walikuwa wakiiba magari
nchini Marekani, wanayapitisha kwa njia za panya kuelekea Mexico na kuyauza
huko.
Hakuwa na jinsi,
japokuwa ilikuwa ni kazi ya hatari iliyohatarisha maisha yake lakini hakuwa na
jinsi, alitakiwa kupambana ili atoke katika umasikini mkubwa uliompigia hodi
mlangoni.
“Ushawahi kuiba
Lambonghin?”
“Hapana!”
“Sasa leo tunakwenda
kuiiba, kama tukifanikiwa, sisi matajiri,” alisema jamaa yake, walikuwa wezi
wakubwa hapo Texas.
“Hakuna noma, ila
hatuwezi kukamatwa?”
“Tutakamatwa vipi?
Kama tumewahi kuiba magari zaidi ya mia tano, tutakamatwaje kwa gari moja?”
aliuliza rafiki yake huyo.
“Basi sawa. Lipo
wapi?”
Huo ndiyo mpango
waliopanga siku hiyo, walitaka kuiba gari ya thamani na kisha kuisafirisha kwa
njia za panya mpaka nchini Mexico. Kuhusu kuiba, hilo wala halikuwa tatizo
kabisa, waliweza kufanya hivyo ila kazi kubwa waliyokuwa nayo mahali hapo ni
kulitoa gari hilo sehemu lilipokuwa na kulipeleka huko walipotaka kulipeleka.
Saa mbili usiku
wakakutana karibu kabisa na ukumbi mmoja wa starehe, mbele yao kulikuwa na
magari mengi lakini miongoni mwa magari hayo, kulikuwa na gari moja la thamani
sana lililokuwa na gharama zaidi ya dola mioni tano, zaidi ya bilioni moja,
ilikuwa lambonghin nyekundu iliyoonekana kuwa mpya kabisa.
Walikuwa wazoefu wa
kuiba magari, hata kuiba gari hilo wala haikuwasumbua kabisa. Kwa sababu Ethan
alikuwa mtaalamu mkubwa wa kuendesha magari, akakaa sehemu ya dereva, kwa kutumia
utundu kwa kuunganisha nyaya, wakaunganisha na gari kuwaka, kilichobakia ni
sauti za watu huko nyuma.
Hapo ndipo walipoanza
safari ya kuelekea mpakani kwa njia za panya ili waweze kuliingiza gari hilo
nchini Mexico. Walipanga kwamba huo ndiyo ungekuwa wizi wao wa mwisho hivyo
baada ya hapo wangeacha kabisa kwani ilikuwa moja ya kazi ya hatari kabisa
kuwahi kuifanya.
“Hivi unakanyaga
mafuta kweli?”
“Ndiyo!”
“Upo ngapi hapo?”
“180 kwa saa!”
“Gari mwisho ngapi?”
“400 kwa saa!”
“Sasa hizo nyingine unamuachia
nani?”
“Ebwana tutakufa.”
“Kama kufa acha tufe,
kuna raha gani ya kuishi, kama kufa tutakufa hata ukiendesha 1 kwa saa, kanyaga
moto kaka,” alisema rafiki yake.
Mwendo aliokuwa
akiendesha ulikuwa ni wa kasi mno, gari lilikuwa likijiweza kwa kasi hivyo
Ethan hakuwa na jinsi, akaanza kukanyaga mafuta mpaka kuhisi kwamba gari hilo
lingeweza kupaa.
Kutokana na kuwa
usiku mwingi, barabarani hakukuwa na magari kabisa, walitembea kwa mwendo
waliotaka tena kwa kasi zaidi na baada ya masaa mawili walitaraji kufika karibu
na mpaka huo ambapo wangechukua njia za panya na kuingia Mexico.
Wakati wamebakiza
kilometa tatu kabla ya kuingia katika kituo cha mafuta cha Gapco, kwa mbali
wakaanza kuyaona magari ya polisi yakiwa yamesimama barabarani huku taa zikiwaka.
Kwanza wakaogopa, kwa
kasi waliyokuwa wakienda nayo walijua kwamba endapo wangeyagonga magari yale
basi ingekuwa kifo chao hivyo alichokifanya Ethan ni kupunguza kasi na
kisha kuchukua barabara nyingine ya vumbi, magari yale ya polisi yakawashwa na
kanza kuwafuata.
“Kanyaga mafuta!”
“Haiwezekani! Hakuna
lami huku,” alisema Ethan.
Walikwenda na gari
hilo kwa umbali mrefu mpaka mafuta yalipowaishia. Hawakuwa na jinsi,
wasingeweza kubaki na wakati polisi waliendelea kuwasogelea kule walipokuwa,
walichokifanya ni kuteremka na kisha kuanza kukimbia huku wakiwa wamelitelekeza
gari lile.
Walikimbia kwa umbali
mrefu, mbele kabisa wakakutana na korongo kubwa, lilionyesha kwamba mchana huwa
kunakuwa na watu wanaochimba kokoto kutokana na ardhi ya Texas kuwa na kokoto
nyingi, walichokifanya ni kuingia katika korongo lile na kuendelea na safari
yao.
Hawakutaka kusimama
sehemu yoyote ile, walichokuwa wakikitaka ni kufika walipotaka kufika pasipo
kugundua kwamba polisi wale wa nyuma walipoona wezi wale kule walipokimbilia,
wakawasiliana na polisi wa mpakani na kuwapa taarifa, nao wakaanza kusogea kule
walipoambiwa wezi wale walipokimbilia, kwa maana hiyo, kadiri Ethan na rafiki
yale walivyokuwa wakipiga hatua, ilikuwa ni sawa na kuwasogelea polisi hao
waliotoka mpakani.
INAENDELEA...