BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 02
Hawakujua kitu
kilichokuwa kikiendelea nje, hawakujua kama kundi la wanawake likiongozwa na mama
mwenye nyumba liliingia ndani na kukisogelea chumba walichokuwa huku wakiwa
wamelaliana kimahaba.
Ghafla, huku wakiwa
wametekwa na uwepo wa mahaba mahali hapo, wakashtukia mlango ukifunguliwa na
kundi zima la wanawake hao kuingia ndani. Kwanza wakashtuka, wakawaangalia
vizuri wanawake wale, alikuwepo mke wake pia.
Mzee Saidi akashtuka,
hakuamini kile alichokuwa kikiona, mdomo wake ukawa mzito kusema chochote kile.
Mkewe alionekana kuvimba kwa hasira, hakuamini kile alichokuwa akikiona
chumbani humo, mume wake ambaye kila siku alikuwa akimuamini ndiye yule
aliyekuwa na mwanamke kitandani kwake, tena mfanyakazi wake aliyemtoa kijijini.
Irakoze alivyoona
hivyo, akaanza kuomba msamaha huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake. Hata
kabla bi Hadija hajazungumza lolote lile, akamvamia msichana huyo wa kazi na
kuanza kumpiga.
Kundi lile la
wanawake halikugobelezea, lilikuwa likishadadia kile kilichokuwa kikiendelea
chumbani pale. Ni mzee Saidi ndiye aliyechukua jukumu la kuanza kuamulia lakini
bi Hadija hakushikika, alikuwa akitukana hovyo.
“Wewe malaya kweli
unaamua kunichukulia mume wangu, tena unalala naye kitandani kwangu, sasa
utanitambua,” alisema bi Hadija huku akimshambulia Irakoze.
“Hadija, hebu muache
mtoto wa watu.”
“Unagombelezea?
Malaya mkubwa wewe, unagombelezeaaaaa?”
Ugomvi ulikuwa
mkubwa, wanawake wale wengine walikuwa wakizungumza maneno yenye kumuumiza
Irakoze juu ya kile alichokuwa amekifanya, kila mmoja alimshutumu huku wengine
wakimpiga masingi na kumzomea.
Irakoze aliumizwa
kutokana na kipigo alichopewa lakini hakuwa na jinsi, kama maji, tayari
yalikwishamwagika na hivyo kufukuzwa nyumbani hapo. Hakutakiwa kukaa, mchana
huohuo akafukuzwa na kuondoka nyumbani hapo huku akilia, furushi la nguo zake
lilikuwa mikononi mwake.
Alijutia kitendo alichokuwa
amekifanya, alianza kujuta kwani kilimuumiza mno. Alipiga hatua kuelekea
Magomeni Mikumi ambapo huko akachukua barabara ndogo iliyokuwa ikielekea Mwembe
Chai kupitia ilipokuwa nyumba ya marehemu Sheikh Yahya.
Alipofika njiani,
mvua kubwa ikaanza kunyesha, hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kwenda kwenye
nyumba moja aliyoiona kufaa na kisha kujikinga na mvua ile iliyokuwa ikinyesha
mno. Hapo ndipo akachukua muda mwingi kuanza kulia,
“Nitakwenda wapi
mimi? Nitakwenda wapi mimi?” alijiuliza huku akilia.
Mvua ilichukua zaidi
ya nusu saa mpaka kuacha kunyesha. Alipoona imeacha, hapo ndipo akalishika
furushi la nguo zake na kisha kusonga mbele. Alikuwa akielekea wapi? Hakujua,
alihitaji kuondoka mbali na nyumba ya mzee Saidi
Alikwenda na
barabara hiyo mpaka alipokuta njia panda, barabara moja ilikuwa ikielekea
Mwembe Chai na nyingine Mburahati, alichokifanya ni kuchukua barabara ya
kuelekea Mburahati ambapo aliamini kwamba angeweza kupata msaada wowote ule.
Alisonga mbele,
furushi lilikuwa kichwani mwake huku akibubujikwa na machozi. Aliona
dunia imemgeukia, hakuwa na pa kukimbilia zaidi ya kwenda mbele kama mtu
aliyekuwa akibahatisha sehemu fulani.
Safari yake iliishia
nje ya nyumba moja, haikuwa ya kifahari, ilikuwa nyumba ambayo kwa kiasi fulani
ilionekana kuchoka. Kulijaa matope lakini hakutaka kujali, kwa kuwa kulikuwa na
kibaraza, akaenda na kutulia hapo.
Kumbukumbu za maisha
yake zikaanza kujirudia kama mkanda wa filamu kichwani mwake, alikumbuka mengi
tangu siku ya kwanza alipofika jijini Dar es Salaam mpaka siku hiyo.
Alihuzunika na kujutia uamuzi wake wa kutembea na mzee Saidi, ila pamoja na
hayo yote, alitakiwa kupambana kwani alijua kwamba huo usingekuwa mwisho wa
maisha yake.
“Habari yako!”
ilisikika sauti ya mwanamke mmoja, alikuwa amefika nyumbani hapo huku mkononi
akiwa ameshika Biblia.
“Salama! Shikamoo
mama!”
“Marahaba binti
mzuri, hujambo?”
“Sijambo!”
Baada ya salamu ile,
mwanamke yule hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kufungua mlango na kuingia
ndani. Irakoze hakutoka kibarazani hapo, aliendelea kukaa huku akionekana kuwa
na mawazo mengi.
Mpaka inafika saa
kumi na mbili jioni, bado hakujua aende wapi, hakuijua vizuri Dar es Salaam
kwani kipindi cha miaka miwili kukaa ndani ya jiji hilo, hakuwa mtembeaji,
alikuwa mtu wa kutulia tu nyumbani, akitoka, kaenda gengeni na kurudi nyumbani.
INAENDELEA...
No comments:
Post a Comment