BIASHARA YA KIFO
sehemu ya 05
Kwa kumwangalia usoni
tu, padri Benedicto alionekana kuhitaji msaada, alitia huruma mno, macho yake
alikuwa ameyapeleka usoni mwa Irakoze huku akionekana kuwa na hofu kubwa. Kile
alichokuwa amekifanya kilikuwa ni kinyume na sheria za kanisa hilo hivyo kama
kanisa lingejua kile kilichokuwa kimetokea, lingekuwa tatizo kubwa.
Hakukuwa na mtu
ambaye angeweza kumsaidia katika kipindi hicho zaidi ya msichana huyo.
Alizungumza naye kwa kipindi kirefu, tena kwa unyenyekevu mkubwa na mwisho wa
siku akamwambia ukweli kwamba alitakiwa kuondoka mahali hapo.
“Niende wapi?”
“Popote pale, ili
mradi utoke ndani ya nyumba hii,” alisema padri Benedicto.
“Kwa hiyo
unanifukuza?”
“Hapana! Sikufukuzi.”
“Ila?”
“Nitakupangia chumba,
utakwenda kuishi huko mpaka utakapojifungua, nakuahidi kukusaidia kwa kila
kitu,” alisema padri Benedicto.
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Hicho ndicho
walichokubaliana, padri hakutaka Irakoze abaki nyumbani hapo kwa kuhofia kwamba
watu wangeweza kujua kwamba alikuwa mjauzito na hivyo mwisho wa siku kumletea
matatizo, alichokifanya ni kumwambia aondoke nyumbani hapo huku akimgawia kiasi
cha shilingi milioni moja.
Kabla ya kuondoka
kwanza akaanza kutafuta chumba ambacho alikipata maeneo ya Sinza Makaburini,
huko ndipo alipoanza maisha yake. Alikuwa akihudumiwa kila kitu na padri huyo,
kuanzia chakula, mavazi, vitu vya ndani na mambo mengine mengi.
Alipewa kiasi cha
shilingi milioni moja kila mwezi kitu kilichompeleka kuanza kufanya biashara
zake binafsi, japokuwa zilikuwa ndogondogo lakini akafanikiwa kwa kiasi kikubwa
kuyaendesha maisha yake.
Katika kipindi hicho
cha kwanza tumbo lake halikuwa likionekana lakini baada ya miezi kadhaa kupita,
kila mtu aliyekuwa akimwangalia alijua kwamba msichana huyo alikuwa mjauzito.
Padri Benedicto akawa
akifika sana nyumbani hapo nyakati za usiku tena huku akiwa amevalia kofia
kubwa ili asiweze kujulikana. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kilikuwa siri
kubwa mno kiasi kwamba hakukuwa na mtu aliyefahamu ukweli.
Baada ya miezi tisa
kukatika, hatimaye Irakoze akajifungua mtoto wa kike aliyempa jina la Annabel
kama ambavyo padri Benedicto alivyotaka aitwe na hivyo maisha yake na mtoto
wake kuanza.
Padri huyo hakukata
mguu nyumbani hapo, kila alipomuona Annabel, moyoni mwake alijisikia furaha
mno, hakuamini kama mwisho wa siku na yeye alifanikiwa na kuitwa baba. Moyoni
mwake alijiona kuwa mwanaume wa shoka, alijikubali japokuwa sheria ya kidini
ilimkataza kuwa na mwanamke yeyote, kuona au kuzaa mtoto.
Siku zaikaendelea
kukatika, hakuacha kufika nyumbani hapo, aliendelea kumlea Irakoze na mtoto
wake na baada ya miaka mitatu kupita huku akiwa amekwishaanza kumjengea nyumba
Irakoze maeneo ya Mbezi Beach, hapo ndipo alipoamua kumwanzisha Annabel Shule
ya Chekechea ya Antonino iliyokuwa Mbezi Beach ambapo wanafunzi wengi walisoma
shuleni hapo walikuwa ni wale waliotoka katika familia za kitajiri.
Mwaka uliofuata
ambapo Annabel aliingia mwaka wa nne hapo ndipo alipoanza kumsumbua mama yake
kuhusu baba yake. Kila siku alikuwa mtoto wa kulia tu, hakukuwa na kitu
alichokuwa akikitamani wakati huo kama kumuona baba yake tu.
“Mama nataka kumuona
baba.....” alisema Annabel kwa sauti ya chini huku akilia.
“Baba yako atakuja.”
“Lini?”
“Kesho! Twende shule
kwanza.”
“Sitaki kwenda mpaka
nimuone baba.”
“Atakuja tu mwanangu!
Twende shule kwanza.”
Japokuwa aligoma
kwenda shule lakini Irakoze hakuwa na jinsi, alimlazimisha Annabel mpaka
akakubali kwenda shuleni. Njiani, alikuwa akilia tu, hakunyamaza, kila
walipofika bado alikuwa akilia kumuona baba yake.
Hicho kilimuumiza
sana Irakoze, kila aliposikia kwamba binti yae mzuri akimuulizia baba yake,
moyo wake ulimuuma mno. Hakuwa na jinsi, alimpigia simu padri Benedicto na
kumwambia ukweli kwamba binti yake alitaka kumuona, hivyo alitakiwa kufanya
kila awezalo aje kumuona.
“Nitakuja.”
“Lini?”
“Sijajua! Ila
nitakuja hivi karibuni.”
“Unajua mtoto wako
anasumbua sana, siku hizi hata kula hataki!”
“Kisa?”
“Anataka kukuona
wewe!”
“Aiseee! Nitakuja
basi.”
“Lini?”
“Kesho usiku!”
“Sawa!”
Siku iliyofuata
usiku, padri Benedisto alikuwa mahali hapo, kitu cha kwanza kabisa alitaka
kumuona binti yake. Japokuwa mara kwa mara alikuwa akifika na kumuona lakini
siku hiyo Irakoze akaamua kumwambia Annabel kwamba yule alikuwa baba yake.
Annabel akafuata na
kumkumbatia, alionekana kuwa na furaha sana na hakutaka kutoka mikononi mwa
baba yake. Kila alipomwangalia binti yake, alifanana naye sana, alijifariji
sana, japokuwa sheria hazikutana padri kuwa na mtoto lakini kwake ilionekana
kuwa furaha kubwa.
Kuanzia siku hiyo,
mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani hapo huku akimkataza Irakoze asimwambie
Annabel kama alikuwa padri kuepuka matatizo hapo baadae. Hilo wala halikuwa
tatizo, Irakoze akakubaliana naye kwamba jambo hilo liendelee kuwa siri siku
zote.
“I will kill you, bullshit,”
(Nitakuua kinyesi cha ng’ombe)
“Do you really want
to kill me?” (Unataka kuniua?)
“Yes!” (Ndiyo!)
“Ok! Just shoot me.”
(Sawa! Nipige risasi)
“I will kill you.”
(Nitakuua)
“Shoot me! Shoot me
right here,” (Nipige risasi, nipige hapa)
Lilikuwa kundi kubwa
la watu zaidi ya thelathini waliozunguka sehemu iliyokuwa na mapipa makubwa ya
uchafu katika mtaa wa kimasikini wa Manhattan uliokuwa katika Jiji la New York
nchini Marekani.
Kila mtu alikuwa
akimwangalia kijana aliyeshika bunduki, alikuwa amemnyooshea mwanaume mmoja,
alionekana kuwa mtu mzima, alikuwa akitamka maneno kwamba angempiga na risasi
endapo tu angeendelea kuzungumza naye mahali hapo.
Kijana huyo
aliyeonekana kuchoka kimaisha aliitwa Ethan Dylan, alikuwa kijana mwenye asili
ya Kingereza ambaye aliishi nchini Marekani. Katika maisha yake yote, hakuwahi
kumuona baba yake, kipindi ambacho mama yake aliondoka nchini Marekani na
kwenda Uingereza ndipo alipokutana na baba yake, akarudi nchini mwao Marekani
ambapo huko ndipo alipokutana na mwanaume aliyeitwa George.
Wawili hao wakapenda
na kuoana. George alikuwa mwanaume mpole, aliyejiheshimu ambaye kila siku
alitamani sana kumuona Ethan akikulia katika maisha mazuri, yenye heshima
ambayo yangemfanya kuwa baba bora miaka ya baadae.
Kutokana na eneo walilokuwa
wakiishi kuwa na vijana wengi wenye fujo, waliojihusisha na madawa ya kulevya,
naye Ethan akajikuta akiingia katika huo mkumbo na mwisho wa siku kuwa mhuni wa
mtaani.
Mama yake aliumia
sana lakini hakuwa na cha kufanya. Kama kuongea, aliongea sana lakini hakukuwa
na kitu kilichobadilika. Baadaye akajiingiza kwenye makundi ya wahuni, huko
akaanza kuuza madawa ya kulevya na mwisho wa siku kumiliki bunduki yake.
Siku hiyo ambayo
alizungukwa na watu wengi, alikuwa amemnyooshea bunduki baba yake wa kambo,
mzee George. Alimwambia ukweli kwamba alitaka kumpiga risasi. Maneno hayo
hayakumshangaza mzee huyo, alichokifanya ni kumsogelea Ethan na kuiweka bunduki
ile kwenye paji lake la uso na kumwambia ampige risasi hapohapo.
“Shoot me right
here,” (Nipige risasi hapa) alisema mzee George, watu wote waliokuwa
wamewazunguka walianza kuogopa kwani walimjua fika Ethan, hakuwa kijana mwenye
masihara, alipokuwa akishinda bastola, hakurudisha nyuma hata mara moja,
alikuwa tayari kuua, pasipo kutegemea, akaikoki bastola yake kitendo
kilichomfanya kila mtu kushtuka mahali hapo. Hata mzee George naye kijasho
chembamba kikaanza kumtoka. Ethan alionekana kukasirika mno, hata mwili wake
ulimtetemeka.
INAENDELEA...
No comments:
Post a Comment