BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 09
Hawakuwa na haja ya gari lile, walikuwa tayari
kuliacha lakini wayaokoe maisha yao, hawakutaka kusimama sehemu yoyote ile,
waliendelea kusonga mbele kwa kuamini kwamba wangefika sehemu iliyo salama
kabisa.
Wakati wamefika
umbali urefu, mara wakaanza kuwaona polisi wakiwa mbele yao, tena wakija kwa
kasi huku wakiwa na bunduki na mbwa walioonekana kuwa na mafunzo makubwa ya
kunusa. Wakati wamebakiza kama hatua mia moja kutoka walipokuwa, wakawaona mbwa
wale wakiongeza kasi ya unusaji wao na kuona kwamba iwe isiwe wangeweza
kukamatwa.
“Tufanye nini? Turudi
tulipotoka au?” aliuliza rafiki yake, Thomson.
“Twende kulia,”
alisema Ethan na kuanza kukimbilia upande wa kulia.
Hiyo haikusaidia,
mbwa wale waliendelea kuwaongoza polisi kule walipokuwa, tayari waliona kwamba
huo ndiyo ungekuwa mwisho wao. Hawakusimama zaidi ya kuongeza kasi zaidi, hiyo
wala haikusaidia kwani kadiri walivyoongeza kasi na ndivyo ambavyo polisi wale
waliokuwa na mbwa walipozidi kuwafuata, tena nao wakiongeza kasi.
“Wooo...wooo...wooo...”
walisikika mbwa wakibweka.
Japokuwa walikimbia
sana tena kwa kasi lakini mwisho wa siku wakajikuta wakikamatwa na kutiwa
nguvuni. Hawakuwa na jinsi, wakabebwa na kupelekwa Jijini Texas ambapo huko
wakafikishwa kituo cha polisi tayari kwa kupelekwa mahakamni.
“Sikutarajia kama
kuna siku ningekamatwa,” alisema Ethan.
“Hata mimi! Ila kosa
lilikuwa pia?”
“Hatukujipanga,
tulikurupuka tu.”
Kesho yake,
wakachukuliwa na kupandishwa mahakamani ambapo huko wakajikuta wakikosa dhamana
na hivyo kupelekwa rumande. Baada ya wiki mbili Ethan na mwenzake wakarudishwa
tena mahakamani ambapo siku hiyo ilionekana kuwa bahati kwao kwani hakukuwa na
shahidi yeyote ambaye alijitokeza na kusema kwamba kweli gari hilo liliibwa, hakukuwa
na mtu yeyote ambaye alisimama kinyume nao na kuweka ushahidi wao ili
wahukumiwe, hivyo mwisho wa siku wakajikuta wameshinda kesi ile.
“Siamini,” alisema
Ethan huku akionekana kutokuamini macho yake.
Wakawa huru, Ethan
akamuahidi rafiki yake huyo kwamba asingeweza kurudia tabia ya kuiba magari
tena kwani kwa kile kilichokuwa kimetokea ni Mungu tu ndiye aliyemsaidia mpaka
kuwa huru muda huo. Baada ya kila kitu kuihs amahakamani, wakatoka nje.
“Samahani,” ilisikika
sauti ya mwanaume mmoja, alikuwa amemshika bega kwa nyuma, Ethan akageuka.
“Bila samahani.”
“Unahitajika!”
“Wapi? Na nani?”
“Kuna mtu anakusubiri
ndani ya gari ile pale.”
“Nani?”
“Twende, utamfahamu
tukifika,” alisema mwanaume huyo.
“Twende Thomason....”
alimwambia rafiki yake.
“Hapana! Unahitajika
peke yako, labda huyu anaweza kusubiri hapa,” alisema mwanaume yule.
Hakuwa na amani
kabisa, alikuwa akijiuliza juu ya huyo mtu aliyekuwa akimsubiri ndani ya gari
lile. Kwa kuliangalia tu, lilikuwa gari la thamani lililomfanya kuona kwamba
mtu aliyekuwa akimiliki gari hilo alikuwa na fedha nyingi.
Hakutaka kusita,
alichokifanya ni kuelekea lilipokuwa gari lile, alipolifikia, mlango
ukafunguliwa na mwanaume yule kisha kuingia ndani. Kulikuwa na giza, hakukuwa
na mwanga, alipokaa kitini, taa zikawashwa na macho yake kutua kwa mwanaume
mmoja, hakuwa mgeni machoni mwake, alimfahamu sana, mara ya kwanza kabisa
alikutana naye ndani ya ndege na kumpa business card yake, na ndiye yule
aliyekuwa akitamani kuwasiliana naye kipindi cha nyuma, alikuwa bwana Boyla
Cook.
“Cook!” aliita Ethan
kwa mshtuko mkubwa.
“Unaendeleaje Ethan?”
aliuliza bwana Cook huku akichia tabasamu pana.”
“Naendelea vizuri,
nilikutafuta sana, nilisahau nilipoiweka business card yako, nimefurahi kuonana
nawe tena,” alisema Ethan huku akionekana kutokuamini.
“Nimefurahi pia.”
Hapo ndipo bwana Cook
alipomwambia kwamba kila kitu kilichoendelea kule mahakamani kilikuwa nyuma
yake, alikuwa amepanga kila kitu na ndiyo maana hata mara ya pili alipofikishwa
mahakamani pale kesi ilikuwa nyepesi sana kwa kuwa alitumia kiasi kikubwa cha
fedha kwa ajili ya kumtoa katika matatizo aliyokuwa nayo.
Ethan akafurahi sana,
akamshukuru mzee huyo lakini hapohapo akaanza kujiuliza juu ya msaada ule, mzee
yule alikuwa akihitaji nini.
“Nashukuru sana! Ila
kwa nini umenisaidia? Na umejuaje kama nilikamatwa?” aliuliza Ethan.
“Nilikuwa
nakufuatilia kila kona, nilikwamba kwamba biashara uliyokuwa ukiifanya haikuwa
salama kwani muda wowote ule ungekuwa kwenye hatari. Nilitamani sana kufanya
kazi na wewe na ndiyo maana kila ulipokuwa, nilihakikisha nakufuatilia kwa
ukaribu.
“Wakati mzee Sanchez
amefariki, nilitaka kuja kukuchukua lakini nilikuwa na safari ya kwenda Brazil,
hivyo nikaamua kuachana nawe kwa muda. Nimerudi siku kadhaa zilizopita na ndipo
nilipotuma vijana wakufuatilie na kujua upo wapi, wakasema umekuja huku Texas
na umekamatwa kwa kosa la kuiba gari na kutaka kulivusha mpakani, hivyo
nikatuma fedha zisaidie kukutoa ili tufanye kazi,” alisema mzee huyo kwa
kirefu.
Ethan akashusha pumzi
ndefu, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, kumbe wakati yeye akijaribu
kukumbuka juu ya kile kikaratasi alichokuwa amepewa chenye namba ya bwana Cook,
kumbe naye alikuwa akimfuatilia kwa ukaribu. Mpaka kufikia hatua hiyo tayari
akajiona kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na bahati kubwa.
“Unataka tufanye kazi
gani?” aliuliza Ethan.
“Twende nyumbani,
tutaongea mengi,” alisema bwana Cook.
“Siwezi kwenda peke
yangu, si unajua nina mwenzangu,” alisema Ethan huku akimwangalia rafiki yake,
Thomson dirishani.
“Mwambie aje,”
aliagiza mzee huyo.
Hapohapo Thomson
akaitwa na kisha kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwa mzee huyo. Kichwa cha
Ethan bado kiliendelea kujiuliza maswali juu ya kazi aliyotakiwa kufanya kwa
mzee huyo. Hakuijua ilikuwa ni kazi gani lakini kwa sababu alionyeshewa msaada
mkubwa, hakuwa na jinsi, alijiona lingekuwa suala la busara kama angekubaliana
naye.
Safari ile ikaishia
mbele ya jumba moja la kifahari, kwa kuliangalia wala usingejiuliza maswali
kwamba jumba hilo lilikuwa likimilikiwa na mtu mwenye fedha, mtu aliyekuwa na
zaidi ya dola bilioni kumi katika akaunti yake. Geti likafunguliwa na kisha
gari kuingizwa.
Lilikuwa jumba kubwa
lililosheheni vitu vyote ambavyo vilitakiwa kuwa ndani ya jumba la bilionea
fulani, kulikuwa na bwana kubwa la kuogelea ambalo sakafu yake ilikuwa ni ya
kioo, kulikuwa na mbuga ndogo ya wanyama na kwa mbali kulionekana kuwa na
wanyama fulani na ndege wengi, kulikuwa na magari ya kifahari na vitu vingine,
ukiachana na hivyo, kulikuwa na masanamu manne ya kike yaliyoonekana kuwa uchi
kabisa.
Milango ya gari
ikafunguliwa na kisha kuteremka, wakaanza kupiga hatua kuelekea ndani. Muda
wote huo Ethan na Thomson walikuwa wakiangalia huku na kule, kila kitu
kilichoonekana kwao kilionyesha ni kwa namna gani bwana Cook alikuwa mtu tajiri
aliyeogelea fedha.
Walipojingia ndani,
kitu cha kwanza kabisa walichokutana nacho ni picha za wanawake wengi
zilizokuwa zimebandikwa ukutani, walikuwa watupu kama walivyozaliwa, walikaa
katika mapozi tofautitofauti na walikuwa wanawake wa kila asili.
Ethan aliziangalia
picha zile, hakuelewa ni kwa nini zilikuwa mahali hapo, ziliusisimua mwili wake
kwani kilipita kipindi kirefu hakuwahi kukutana kimwili na mwanamke yeyote
yule. Alizunguka huku na kule, macho yake yalikuwa yakiangalia kila kona.
“Mbona kuna picha
nyingi sana za wanawake?’ aliuliza Ethan.
“Ninapenda kuwa
nazo.”
“Ndiyo ziwe nyingi
namna hii?”
“Yeah! Huwa
ninafurahia ninapomwangalia mwanamke akiwa mtupu.”
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo!
Karibuni sana,” alisema bwana Cook huku akiachia tabasamu pana.
Wakakaa kwenye
makochi ya manyoya na kutulia. Wote wawili walikuwa wakiangalia huku na kule,
bwana Cook akatoka sebuleni hapo na kuelekea chumbani kwake, baada ya dakika
tatu akarudi huku akiwa amebadilisha nguo zake, akaagiza vinywaji, vikaletwa na
kuanza kunywa.
“Ninataka unifanyie
kazi Ethan,” alisema bwana Cook.
“Kazi gani?”
“Kwanza unajua mimi
ni nani?”
“Unaitwa Boyle Cook,
sijui kingine zaidi ya hicho,” alijibu Ethan.
“Sawa. Hujawahi
kulisikia jina langu sehemu yoyote?”
“Hapana!”
“Mimi ni mkurugenzi
wa kampuni ya kutengeneza filamu za utupu ya Bravilian.sex, ni kampuni
inayojitegemea na ambayo imetengeneza filamu nyingi mno,” alisema bwana Cook.
“Sawa! Nimefurahi
kukufahamu! Kwa hiyo unataka na mimi niigize?”
“Ungependa kuigiza?”
“Hapana! Siwezi
kabisa.”
“Sawa! Lengo la
kukuita hapa si kutaka uigize bali kuna kazi nyingine nataka uifanye,” alisema
bwana Cook.
“Kazi gani?”
“Kunitafutia
wasichana wengi duniani kwa ajili ya kuigiza, kila msichana nitakulipa dola
elfu kumi,” alisema bwana Cook.
“Mmmh!”
“Ni kazi ngumu?”
“Si sana, kama
nitapewa fedha za kutosha kuzunguka duniani, si kazi ngumu, hakuna tatizo,”
alisema
“Ila kuna kazi
nyingine nataka ufanye, ila kwa siri sana.”
“Kazi ipi?”
“Biashara ya Kifo,”
alisema bwana Cook, Ethan na Thomson wakashtuka.
INAENDELEA...
No comments:
Post a Comment