Sunday 21 January 2018

HADITHI!!......... HADITHI.................

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 01:

Imetungwa na Nyemo Chilongani

Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha, mitaro midogo ikaanza kujaa maji huku baridi likianza kupiga kwa nguvu ndani ya jiji la Dar es Salaam. Waliokuwa ndani ya nyumba zao, wakajifungia huku wale waliokuwa barabarani wakinunua miamvuli kwani mvua ile kubwa haikuonekana kuwa na dalili za kupungua hata mara moja.

Watu wengine walikuwa wakikimbilia sehemu zilizokuwa na uwezo wa kuzuia wasilowanishwe na mvua hiyo, wengine, walikubaliana na kile kilichokuwa kikiendelea hivyo kuendelea na kazi zao au safari zao huku wakiendelea kulowa.
Nje ya nyumba moja kubwa, msichana mrembo, mwenye sura nzuri, aliyekuwa na umbo lenye mvuto ambalo vijana wa sasa wangeliita namba nane alikuwa amesimama huku mkononi mwake akiwa ameshika furushi la nguo lililokuwa na nguo nyingi zilizofungwa kwa khanga.

Pale alipokuwa, macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa na kitu moyoni mwake, hakuonekana kuwa mwenye furaha hata mara moja, baada ya dakika chache, machozi yale yaliyojikusanya machoni mwake yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Msichana huyu aliitwa kwa jina la Irakoze, baba yake alikuwa Mrwanda na mama yake alikuwa Mnyaturu kutoka mkoani Singida. Historia ya maisha yake ilianzia mbali, miaka miwili iliyopita, alikuwa akiishi mkoani Singida ambapo baadaye mwanamke aliyeitwa kwa jina la Hadija aliyetoka jijini Dar es Salaam akafika kijijini kwao na kumchukua kwa lengo la kwenda kufanya kazi katika nyumba yake iliyokuwa Magomeni jijini Dar.

Hilo ndilo lilikuwa lengo lake, aliporuhusiwa kumchukua, akaenda naye Dar ambapo huko baada ya kuishi kwa mwezi mmoja tu, wanaume wakaanza kumtongoza kwani ule urembo aliokuwa nao ulimvuta kila mtu aliyekuwa akimwangalia.
Uoga ulimjaa moyoni mwake, maneno aliyopewa na bi Hadija kwamba kama angefanya ujinga na wanaume hao basi angefukuzwa na kurudishwa kijijini, ukamuogopesha na hivyo kila mwanaume aliyemfuata, alimwambia kwamba hamtaki.
Ilimsaidia, aliendelea kunawiri kila siku lakini baada ya mwaka na miezi minne kukatika, mume wa bi Hadija, mzee Saidi akashindwa kuvumilia, umbo matata alilokuwa nalo Irakoze likamchanganya, kila alipokuwa akimuona, akashindwa kuvumilia, hivyo akaanza kumzengea.
Visa vikaanza, mzee Saidi akashindwa kuvumilia, umbo la msichana yule na sura yake vilimchanganya mno hivyo kuanza harakati zake ndani ya nyumba. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuomba likizo kazini, alitaka awe anabaki nyumbani na binti huyo afanye yake wakati mkewe akiwa kazini.
“Unaogopa nini Irakoze? Hebu sogea hapa kitandani,” alisema mzee Saidi, pepo la ngono lilimshika, hakutaka kuelewa kitu chochote kile, mwili wake uliwehuka, kila alipomwangalia Irakoze, alimchanganya, umbo lake, makalio yake yaliyojaajaa yalimuacha hoi, hakutaka kukubali.
“Sitaki baba, sitaki,” alisema Irakoze huku akijifanya kubisha mlangoni alipokuwa amesimama, cha ajabu, hakutaka kutoka chumbani humo.
Mzee Saidi hakutaka kulaza damu, tayari aliona kila kitu kilikuwa sawa japokuwa hakuweka usiriazi katika kumlaghai msichana huyo kuja kitandani pale alipokuwa, alichokifanya ni kusimama na kuanza kumsogelea, alipomfikia, akamshika mkono na kuanza kumvutia kwake, muda wote huo Irakoze alikuwa akiangalia chini, uso wake ulijawa na aibu mno.
“Naogopa baba,” alisema Irakoze.
“Unaogopa nini?”
“Mama atajua.”
“Atajuaje? Utamwambia?”
“Hapana!”
“Sasa atajuaje?”
Irakoze akakosa jibu, ukimya wake ulikuwa ni kama jibu lililomruhusu mzee Saidi kufanya kile alichotaka kukifanya, akamvuta, msichana huyo, akaanza kupiga hatua kuelekea kitandani, kilichofauata ni kufanya mapenzi kitandani hapo.
Huo ulikuwa mwanzo wa kudokoa asali, baada ya hapo, wakajikuta wakiingia kwenye dimbwi zito la mahaba, kila siku mzee Saidi alipokuwa akiamka, mtu wa kwanza aliyetaka kumuona alikuwa Irakoze tu.
Penzi la msichana huyo likamlevya, hakutaka kusikia chochote kile, alichokuwa akikitaka ni mapenzi motomoto tu. Hata mzee Saidi aliporudi kazini, kuna siku alikuwa akitoroka kazini na kurudi nyumbani, huko, alikuwa akifanya mapenzi na msichana huyo tu.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba kilikuwa siri kubwa, bi Hadija hakugundua chochote kile kwani maigizo waliyoyafanya wawili hao yalimpigwa upofu mkubwa, hakujua kama nyuma ya pazia alikuwa akiibiwa.
“Lakini nilikwambia simuni mke wangu!” alisema mzee Saidi, alikuwa kilalamika.
“Najua mume wangu, ila nikasahau kabisa kumwambia Irakoze kama ulikuwa ukihitaji upikiwe samaki,” alisema bi Hadija.
“Aiseee! Sasa hapa kuna umuhimu wa huyu msichana kumnunulia simu, vinginevyo kuna siku tunaweza kugombana kitu ambacho sitaki kitokee,” alisema mzee Saidi.
Hiyo ndiyo ilikuwa mbinu aliyoitumia, alitaka kuwasiliana na Irakoze kwa karibu mno, kitendo cha kurudi nyumbani ghaflaghafla kingemfanya siku kukutana na mke wake nyumbani hapo hivyo kufumwa, alichokitaka ni kuwasiliana na msichana huyo tu.
Bi Hadija hakujua, kwa fedha zake, akanunua simu na kumpa Irakoze pasipo kujua kwamba ndiyo kwanza aliliua pendo lake kwa mume wake. Hiyo ikawa nafasi nzuri kwa mwanaume huyo kuwasiliana na Irakoze ambapo kama bi Hadija hakuwepo nyumbani, walikumbatiana, walibusaiana na kupetiana kama kawaida yao.
“Siku mama akijua!”
“Unahisi atafanyaje?”
“Atanifukuza.”
“Hawezi! Mimi ndiye kidume humu ndani!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Hebu sogea kwanza unibusu hapa,” alisema mzee Saidi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimpenda kama mume wake, alimwamini sana kwani katika miaka yao kumi na tano ya ndoa hakuwahi kusikia hata siku moja akitoka nje ya ndoa yao. Alimthamini na kujiona amepata mume wa ukweli, mume aliyejua kulea na kupenda.
Siku ya kwanza aliposikia tetesi kwamba kulikuwa na uwezekano wa mume wake kutembea na mfanyakazi wake, alibisha sana na kuona kwamba watu walitaka kuivunja ndoa yao iliyodumu kwa kipindi kirefu.
Masikio akayaziba pamba, hakutaka kusikia chochote kile kutoka nje. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, tetesi zile zilizidi kuvuma kiasi kwamba akahitaji kuhakikishakwa macho yake, hakutaka kusikia tena hivyo kuanza mishemishe kwa kuwaweka walinzi ili siku mume wake akitoroka kazini, apigiwe simu.
“Nitakupigia tu shosti wangu! Mimi tena nishindwe! Hata ukitaka nivae dela wakati wa kwenda kufumania, nipo radhi na kikundi changu cha msuto,” alisema mwanamke ambaye kila siku alikuwa akimsisitizia kwamba alikuwa akichangia mapenzi yake na msichana wake wa kazi.
Siku zikaendelea kukatika, ilikuwa ni kama watu hao wamejua vile, mzee Saidi hakuwa akirudi nyumbani. Wanawake wa mtaani walizidi kusubiri lakini mzee huyo alisitisha zoezi lake la kutoroka kazini na hivyo kutulia hukohuko.
Baada ya mwezi mmoja kupita, mzee Saidi akaonekana akianza kuelekea nyumbani kwake, kama kawaida yake gari lake alilipaki mbali na nyumbani hapo ili hata mkewe akirudi, asiweze kujua kama alikuwa ndani.
“Shoga! Amekuja. Njoo haraka,” aliongea mwanamke huyo, alikuwa akimwambia bi Hadija simuni.
Wala hazikupita dakika nyingi, bi Hadija akafika mahali hapo. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili ulimtetemeka kwa hasira, alichokuwa ameambiwa, kilimtia hasira mno, akajikuta akiwa na presha kubwa ya kuingia ndani kwa lengo la kufumania.
“Subiri kwanza,” alisema mwanamke huyo, tayari wanawake wenzake walikwishakusanyika mahali hapo.
“Nina presha, niacheni niende.”
“Usiwe na presha. Ngoja kwanza tuvae madela yetu,” alisema mwanamke huyo huku wanawake waliokuwa mahali hapo wakienda makwao na kuanza kuvaa madela tayari kwa kufumania.
Wakati mambo yote hayo yakiendelea, kama kawaida, ndani ya nyumba, Irakoze na mzee Saidi walikuwa chumbani kama walivyozaliwa, walikuwa wakipeana mapenzi motomoto pasipo kujua kwamba wakati mzee huyo akiingia ndani na kupokelewa kwa mabusu mfululizo, walisahau hata kufunga mlango.
Wanawake hao wakaingia ndani na kuanza kuelekea chumbani. Mwendo wao ulikuwa ni wa kunyata huku bi Hadija akiwa na hasira mno.


ITAENDELEA...

No comments:

Post a Comment