BIASHARA YA KIFO
SEHEMU YA 7.
“Ethan, stop,” (Ethan, acha) ilisikika
sauti ya mama yake kutoka nyuma.
Ethan hakutaka
kuiachia bunduki ile, alikuwa amedhamiria kumuua baba yake wa kambo, hakumpenda
kabisa, alimchukia mno, kitendo cha kumuona kila siku katika maisha yake
kilimkasirisha.
Alijiandaa
kumfyatulia risasi na kumuua kabisa, lakini hata kabla hajafanya hivyo, mama
yake akamsogelea na kisha kumzuia kubonyeza kitufe cha bunduki ile. Hiyo
ikaonekana kuwa bahati ya mtende kwa mzee George, kwa jinsi alivyomwangalia
Ethan, alikuwa amedhamiria kumuua kabisa.
Ethan akaondoka
mahali hapo, kundi lile la watu lililokuwa limewazunguka nao wakaondoka
kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Hayo ndiyo yalikuwa
maisha yake, alichukiwa na kila mtu kwa kuwa alikuwa mtemi, japokuwa alikuwa na
miaka kumi na sita lakini tayari Ethan alijifunza maisha ya mitaani hasa ya
kutumia bunduki katika maisha yake.
Alikuwa mtu wa fujo,
alijulikana sehemu kubwa hapo Manhattan huku akianzisha kundi lake kubwa la
kihuni lililojulikana kama The Mobb. Lilikuwa na vijana ishirini,
walioshindikana katika maisha yao, walikuwa watumiaji wazuri wa bunduki,
walikuwa wavuta bangi na hata wakati mwingine kutumia madawa ya kulevya.
Walikuwa vijana
wadogo lakini wale ambao hawakuwa na huruma hata kidogo. Polisi wa hapo
Manhattan waliliogopa kundi hili, hawakuyathamini maisha yao, kwao, kupigwa
risasi na kufa lilikuwa jambo jema tu kwani waliamini kwamba kulikuwa na mungu
wao wa kisela ambaye angewpokea nakuwaingiza katika mbingu yao iliyokuwa na
makontena makubwa ya madawa ya kulevya na bangi.
Wakati kundi hilo
likiendelea kukua, likiwapiga watu na hata wakati mwingine kuwaua, hapo ndipo walipotumwa
polisi waliokuwa na hasira, polisi waliotoka nje ya Manhattan kwa ajili ya
kufanya jambo moja tu, kuwakamata vijana hao na hata kama wataleta ubishi au
kufanya chochote kilicho kibaya cha kuhatarisha maisha yao, basi wawaue.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo
wa kumaliza magenge hayo, vijana wengi walikamatwa na kufungwa gerezani lakini
kwa Ethan, akatoroka jijini New York na kuhamia Washington DC ambapo maisha
yake yakaendelea.
Hakutaka kuwa mhuni
kama alivyokuwa, hakutaka kufanya usela wa mitaani alichokifanya kwa wakati huo
ni kujikita katika uuzaji wa madawa ya kulevya kwa kuyasafirisha sehemu moja
kwenda nyingine.
Hapo ndipo
alipokutana na wale watu aliokuwa akiwasikia kwamba walikuwa wauzaji wazuri wa
madawa ya kulevya na walikuwa watu wenye kuogopwa sana. Alipofikishwa kwa mzee
mmoja aliyekuwa na asili ya Mexico, mzee Sanchez El Paso, akamchukua na
kumfanya mfanyakazi wake ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafirisha madawa
nchini Marekani.
“Ukifanya kazi na
mimi, utakuwa tajiri mno,” alisema mzee Sanchez.
“Nitatajirika vipi?”
“Utafahamiana na watu
wengi, nisingependa ufanye kazi kwangu milele, pia ningependa baadaye ufanye
kazi wewe kama wewe,” alisema mzee Sanchez.
“Ili nifikie ndoto ya
kufanya biashara zangu mwenyewe, natakiwa kufanya nini?”
“Kujitoa kazini,
hakuna cha zaidi, ila epuka sana wizi, ukiiba na kugundulika, nitakuua,”
alisema mzee huyo maneno yaliyomtia hofu mkubwa.
“Siwezi kufanya
hivyo! Umenitoa mbali, hakika nitaendelea kukuheshimu na sitokufanyia ujinga,”
alisema Ethan.
Alimheshimu mzee huyo
kwa kuwa ndiye aliyekuwa akimfanyia mambo mengi na kukutana na watu ambao
hakutegemea kukutana nao katika maisha yake. Kila siku alikuwa mtu wa kutoka,
hakutulia sehemu moja, leo alikuwa akienda California, kesho Texas na kesho
kutwa sehemu nyingine.
Hayo ndiyo yalikuwa
maisha yake, kila siku alikuwa akibadilisha muelekeao wake ambapo kote huko
kazi kubwa aliyokuwa akiifanya ni kusafirisha madawa ya kulevya tu. Jina lake
likaanza kukua, mnyororo mkubwa aliokuwa nao mzee Sanchez ukamsaidia mno na hata
katika viwanja vya ndege mbalimbali hakuwa akipata usumbufu wowote ule.
“What do you want?”
(Unataka nini?) aliuliza mzee mmoja.
“What do I want? What
do you mean?” (Nahitaji nini? Unamanisha nini?)
“For how long have
you been doing this work?” (Kwa kipindi gani umekuwa ukifanya kazi hii?)
“Three years?” (Miaka
mitatu)
“Ok!” (Sawa)
Alikuwa akizungumza
na mzee mmoja aliyekuwa amekaa naye ndani ya ndege. Hakujua ni nani alimwambia
kuhusu biashara ya madawa ya kulevya aliyokuwa akiifanya, mzee huyo alianza
kumuuliza maswali mengi kiasi kwamba akaanza kuogopa kwani hata humo ndani ya
ndege alipokuwemo, alikuwa na mzigo mkubwa aliokuwa akiupeleka Los Angeles.
“Lakini wewe ni
nani?” aliuliza Ethan huku akionekana kushikwa na hofu.
“Ninaitwa Boyle
Cook,” alijibu mzee yule.
“Umejua vipi kama
ninafanya kazi hii?”
“Hauwezi kunificha,
ninawajua kwa kuwaangalia, umekuwa na amani katika kufanya kazi hii?” aliuliza
bwana Cook.
“Kiasi, si sana,
wakati mwingine unakuwa na hofu kubwa.”
“Utakuwa tayari kama
nikikupa kazi nyingine, nzuri tu?”
“Kazi gani?”
“Ninataka uwe na
amani, siwezi nikakupa kazi ngumu. Niambie, upo tayari?” aliuliza bwana Cook.
“Mmmh!”
“Usijali! Chukua hii,
ukiwa tayari niambie,” alisema bwana Cook na kisha kumpa business card yake
iliyokuwa na mawasiliano yote.
Mpaka kufikia hatua
hiyo Ethan alichanganyikiwa, alikuwa akimwangalia mzee huyo mara mbilimbili,
hakumfahamu alikuwa nani, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana naye, tena
walizungumza kwa muda mchache kabla ya mzee huyo kubaki kimya mpaka ndege
ilipotua Jijini Los Angeles na kisha kuteremka.
Hawakuzungumza
chochote kile, kila mmoja akaendelea na kazi zake zilizomleta ndani ya jiji
hilo la starehe. Ethan akaondoka na kupeleka mzigo alipoelekezwa kwani hata
kuutoa pale uwanja wa ndege hakukuwa na kazi kubwa kwani kila kitu kiliwekwa
tayari.
Kichwa chake kikawa
na maswali mengi, alikuwa akijiuliza kuhusu mzee yule ambaye alionekana
kumfahamu mno, hakuishia hapo, aliendelea kufikiria hata ile kazi aliyotaka
kumpa, hakujua ilikuwa kazi gani ila alimwambia kwamba endapo angekuwa tayari
basi amtafute.
Uuzaji wa madawa ya
kulevya ilikuwa biashara mbaya na yenye hatari mno lakini hakutaka kuiacha
kwani ilimpa kisasi fulani cha fedha na kuanza kuyabadilisha maisha yake.
Alichokifanya ni kumpuuzia bwana Cook na yeye kuendelea na maisha yake kama
kawaida ingawa mara nyingi mno alikuwa akijiuliza kuhusu mzee yule na kukosa
jibu.
INAENDELEA...
No comments:
Post a Comment