BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 10
Ni kweli walishtuka,
hawakuamini kile walichokisikia kwamba mbali na kuwatafuta wanawake waliotakiwa
kuwapeleka kwa ajili ya kuigiza filamu, kulikuwa na kazi nyingine ya ziada
ambayo iliitwa Biashara ya Kifo.
“Ndiyo inakuwaje
hiyo?”
“Ni kazi rahisi tu
japokuwa unahitajika umakini wa hali ya juu,” alisema bwana Cook.
Hapo ndipo mzee huyo
alipoanza kueleza namna ambavyo biashara hiyo ilitakiwa kufanyika. Kulikuwa na
kundi la wanawake mitaani waliokuwa wakihitaji ajira, watu waliokuwa wakitafuta
ajira kila siku, mbali na hiyo, kulikuwa na kundi kubwa la wanawake ambao kila
siku walitamani kufika nchini Marekani.
Hao ndiyo waliotakiwa
kufanyiwa biashara hii. Kazi ilikuwa ni kuwafuata na kuanza kuwalaghai kwa
maneno matamu kwa kuwaahidi kwamba wangewapa ajira yenye kiasi kikubwa cha
fedha na hivyo wawasafirishe kwenda nchini Marekani, wanapofika huko,
walazimshwe kuigiza filamu za ngono, kwa atakayetaka kuendelea basi aendelee
lakini kwa wale ambao wangekataa kuendelea na kulilia kurudi nyumbani, basi hao
wauawe na kisha kuchunwa ngozi ambayo ingepelekwa nchini China kwa ajili ya
kutengenezea vitu vya asili.
“Mmmh!” aliguna
Ethan.
“Unahisi ni kazi
ngumu?”
“Kwangu! Kuchuna
ngozi ya binadamu, sijawahi kufanya kazi hiyo,” alijibu Ethan.
“Kazi yako si kuchuna
ngozi, kazi yako kubwa ni kutafuta wasichana tu, hakuna jingine, hiyo ni kazi
ya watu wengine,” alisema bwana Cook.
“Kama ndiyo hivyo,
hakuna shida.”
Hiyo ndiyo kazi
aliyoahidiwa kulipwa kiasi kikubwa cha fedha. Kilichofanyika ni kupewa kiasi
cha dola elfu hamsini ambazo zilikuwa ni zaidi ya milioni hamsini,
akatengenezewa pasipoti kubwa kwa ajili ya kusafiria nchi hadi nchi na kisha
kuanza safari za kuwatafuta wasichana kwa ajili ya kuigiza filamu za ngono.
Safari yao ya kwanza
kabisa kwenda ilikuwa nchini Hispania, huko wakakutana na wasichana kadhaa na
kuhitaji kufanya nao mahojiano kwa ajili ya kazi za uongo walizowaambia kwamba
zilikuwa nyingi nchini Marekani.
“Upo tayari?”
“Kiasi gani?”
“Dola elfu moja kwa
siku,” alijibu Ethan.
“Mmmh! Ni kazi gani?”
“Zipo nyingi tu
lakini unatakiwa kuchagua. Kuna kazi za hotelini, kupika na nyingine nyingi,”
alisema Ethan.
“Nipo tayari!”
“Sawa.”
“Si umesema Marekani?”
“Ndiyo!”
“Hakuna tatizo!”
Kutokana na wimbi
kubwa la wasichana wa Ulaya kukosa ajira na kutamani sana kwenda nchini
Marekani kwa kuamini kwamba kulikuwa na maisha mepesi, wakakubaliana na Ethan
na mwisho wa siku kuelekea huko.
Ishu zote za usafirishaji
zilikuwa chini yake, alitumia kiasi kikubwa cha fedha alichopewa na bwana Cook
hivyo hakukuwa na tatizo lolote lile. Walipofika nchini Marekani katika Jiji la
New York ambapo ndipo kulipokuwa makao makuu ya kampuni hiyo ya filamu za
utupu, wakapelekwa hotelini na kuambiwa wasubiri.
“How many are they?”
(Wapo wangapi?)
“Ten young girls!”
(Wasichana wadogo kumi)
“What do you mean?
Below 18?” (Unamaanisha nini? Chini ya miaka kumi na nane?) aliuliza bwana
Cook.
“No! Above 18 but
below 23,” (Hapana! Zaidi ya miaka 18 lakini chini ya miaka 23)
“Ok!” (Sawa)
Mara baada ya kufika
katika hoteli hiyo, wakaambiwa waoge kwa ajili ya chakula cha usiku na siku
inayofuata wangeanza safari ya kuelekea katika eneo la kazi, kule walipotakiwa
kufanya kazi.
Kila mmoja alikuwa na
furaha mno, kutoka nchini Hispania mpaka kufika nchini Marekani, tena kufanya
kazi ndogo kwa mshahara mkubwa ilionekana kuwa kama bahati kwao. Sheria moja
kubwa waliyokuwa wamepewa ni kutokutumia simu tu.
Waliufurahia usiku
huo kwa kuona kwamba ndiyo ilikuwa mwanzo wa safari yao ya kuwa mamilionea mara
watakaporudi nchini mwao, hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba nyuma ya pazia
kulikuwa na zoezi zima la kuigiza filamu za utupu na kama kungekuwa na yeyote
atakayekataa basi ilikuwa ni lazima auawe na kuchunwa ngozi.
“Andikisheni majina
yenu na nafasi unazotaka kufanya kazi,” alisema Ethan, alikuwa akiwaambia
wasichana hao kumi ambao wakafanya kama walivyotakiwa kufanya.
Siku iliyofuata Ethan
akarudi hotelini hapo kisha kuwachukua, akawapeleka katika jumba moja kubwa
lililokuwa pembezoni mwa Jiji la New York, aliwaandaa kwa ajili ya kazi
aliyotaka kuwapa. Kwa kuwaangalia wasichana wale, walionekana kuwa na furaha
kubwa kwa kuamini kwamba huo ungekuwa mwanzo tu kwani hata mapokezi waliyokuwa
wamepewa siku hiyo yalikuwa makubwa na ya kifahari.
Wakateremka kutoka
garini na kuingia ndani ya jumba moja kubwa, humo wakaambiwa watulie kwani
kulikuwa na mtu aliyetaka kuzungumza nao. Wakatulia vitini na Ethan kuelekea
chumbani. Baada ya dakika moja akarudi na mwanaume mmoja, alikuwa mtu mwenye
umri mkubwa ambapo kwa kumwangalia tu, ungehisi kwamba alikuwa na miaka zaidi
ya hamsini.
“Karibuni sana,”
aliwakaribisha mzee huyo.
“Asante sana,”
waliitikia kwa pamoja.
“Mpo hapa kwa ajili
ya kufanya kazi, si ndiyo?”
“Ndiyo!”
“Kazi ipo, ila
mmekwishaambiwa ni kazi gani mtakayofanya?”
“Hotelini!”
“Sawa! Ila kwa bahati
baya huko kazi imekwisha, iliyobakia ni moja tu,” alisema mzee huyo ambaye
alijitambulisha kwa jina la Gregory.
Wasichana wale
walipoambiwa kwamba kazi ya hotelini ambao walikuwa wameifuata ilikwisha, kila
mmoja akanyong’onyea lakini walipoambiwa kwamba kulikuwa na kazi nyingine
ambayo ilikuwepo mahali hapo, wakarudi kwenye tumaini jipya.
“Kazi gani?”
“Mnajua kuigiza?”
“Mimi najua...” alisema
msichana mmoja.
“Hata mimi najua,”
alisema mwingine, mwisho kabisa, wote walisema wanajua.
“Nani anamjua Blue
Diamond?”
“Mimi simfahamu.”
“Mimi namfahamu! Ni
mcheza filamu za utupu,” alijibu msichana mmoja.
“Sawasawa! Blue
alikuwa msichana kama nyie, wakati alipotoka nchini Canada, alifikia ndani ya
nyumba hiihii, alikuwa masikini sana, lakini tukayabadilisha maisha yake na
kuwa tajiri namna hiyo. Tulipomwambia kuhusu kuigiza filamu hizo, aliogopa sana
lakini sasa hivi anatushukuru na kutulaumu kwa kuwa tulimchelewa kumwambia juu
ya mafanikio makubwa ambayo angeyapata.
“Sasa hivi Blue ni
msichana mwenye mafanikio, anaoglelea kwenye bwawa la fedha, anaendesha gari
analotaka. Wangapi mpo tayari kuwa kama Blue?” alisema mzee Gregory na
kumalizia na swali.
“Kuwa muigizaji wa
filamu za utupu?” aliuliza msichana mmoja.
“Ndiyo!
Hatukulazimishi kuigiza, hakuna mtu anayelazimishwa kuyafuata mafanikio na
utajiri. Huwa tunalipa dola elfu tatu kwa kila kipande kimoja kwenye filamu
zetu, kwa maana hiyo ikitokea ukafanya mapenzi na wanaume wawili kwa mpigo,
utapata dola elfu sita,” alisema mzee huyo.
Kiasi cha fedha
ambacho walitajiwa kilikuwa kikubwa mno zaidi ya milioni sita kwa mtu mmoja na
milioni kumi na mbili kama utafanya mapenzi na wanaume wawili kwa pamoja, kila
aliyekisikia, alitamani kukipata hapohapo lakini tatizo likawa namna ya kuigiza
filamu hizo. Wasichana hao wakaanza kutoa minong’ono ya chinichini lakini
mzee yule aliendelea kuwaambia kwamba ilikuwa ni lazima wafikie mafanikio kama
wangekubaliana nae.
Ili kuendelea
kuwalaghai, wakawaletea mikataba na kuwawekea mbele yao, walitakiwa kusaini
kisha kuandika akaunti zao ili mara watakapoanza kuigiza basi wawekewe kiasi
hicho cha fedha.
“Mimi sipo tayari,”
alisema msichana mmoja.
“Hata mimi sipo tayari,”
alisema msichana mwingine.
“Sawa! Hakuna
tatizo!”
“Mimi nipo tayari!”
“Safi sana!”
Kati ya wasichana
kumi, wanne walikuwa tayari, wakakubaliana na mzee Gregory kisha kuambiwa
wabaki mahali hapo huku wale sita waliokataa wakiambiwa warudi hotelini tayari
kwa kujiandaa na safari siku ijayo kurudi nchini Hispania.
Wakasimama na
kutolewa nje, wakaingizwa ndani ya gari huku Ethan akiwa pamoja nao. Gari
halikwenda hotelini, lilibadilisha njia na kwenda katika jumba jingine kabisa,
wao wenyewe walishangaa, hawakujua waliletwa pale kwa ajili gani, wakashushwa
na kuingizwa ndani ya jumba lile, lengo kamili lilikuwa ni kuuawa na kisha
kuchunwa ngozi, hiyo ndiyo ilikuwa Biashara ya Kifo, walitakiwa kuuawa na ngozi
zao kutumwa nchini China ambapo kulikuwa na biashara nzuri tu.