Wednesday, 24 January 2018

HADITHI!!!......SEHEMU YA SITA

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 06


Maisha yaliendelea kama kawaida. Hakukuwa na kitu kilichokisumbua kichwa cha padri Benedicto kama kumuona mzazi mwenzake akiishi mbali naye. Hakuwa na uwezo wa kwenda kukaa naye lakini kila siku alikuwa mtu wa kutamani kumuona mwanamke huyo akiwa karibu naye kwani ndiye mtu pekee aliyeonekana kuwa faraja katika maisha yake.
Kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo juu yake, muda wote alihisi kwamba alikuwa akiibiwa tu. Aliwafahamu vijana wa Sinza, walikuwa vijana makini kuhusu masuala yote ya mapenzi, walikuwa na uwezo mkubwa wa kumteka msichana yeyote hata kama angekuwa mgumu kiasi gani.
Hakutaka kusalitiwa, alitaka Irakoze awe wake peke yake, hivyo alichokifanya ni kuanza kupanga mipango kabambe ya kumbana mwanamke huyo kwa kumpeleka katika Chuo cha Utawa,  St. Mary’s Catholic kilichokuwa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam na kuingia pale kama mpishi.
Mipango yote ya Irakoze kuingia ndani ya chuo kile ilifanywa na padri Benedicto huku akimchukua Annabel na kumpeleka nchini Marekani kwa ajili ya kusoma huko katika Shule ya Consolatha Seminary School iliyokuwa katika Jiji la New York nchini Marekani.
Kidogo moyo wake ukawa na amani, kutokana na umbo lake kuwa dogo na sura ya kitoto aliyokuwa nayo, mara baada ya kufika katika chuo hicho cha Utawa, masista wote walihisi kwamba Irakoze alikuwa msichana mdogo, hivyo wakamchukulia hivyohivyo.
Kila siku alikuwa hapo huku akiwasiliana na padri Benedicto simuni, bado wawili hao waliendelea kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa siri sana kiasi kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyefahamu kilichokuwa kikiendelea.
Huo ulikuwa mwaka wake wa kwanza chuoni hapo, alionekana kuwa mtu mwenye heshima, alimheshimu kila mtu kuanzia wale wa chini mpaka wa juu. Wasichana wengi waliokuwa chuoni hapo walimpenda Irakoze ambaye walipenda kumuita kwa jina la Sista Magdalena.
Siku zikaendelea kukatika, kila alipokuwa akitumwa mjini kwa ajili ya kununua baadhi ya vitu kwa ajili ya shule hiyo, alikuwa akienda na kuonana na padri Benedicto na kisha kulala wote hata kwa masaa mawili kisha kurudi chuoni.
Huko ndipo alipopata taarifa kuhusu binti yake aliyekuwa nchini Marekani. Masomo yaliendelea vizuri na mara kwa mara safari za Benedicto kuelekea nchini Marekani hazikuisha, kila alipokwenda, alihakikisha anaonana na binti yake na kisha kurudi nchini Tanzania.
“Amekua sana, mwaka wa sita huu,” alisema Benedicto, alikuwa akimwambia Irakoze.
“Nina kiu ya kumuona.”
“Usijali! Ila nataka tuifanye kitu kimoja”
“Kipi?”
“Na wewe usomee utawa!”
“Mmmh!”
“Hakuna tatizo! Utafanikiwa tu, nataka uwe na safari za kutosha kwenda Ulaya na sehemu nyingine,” alisema Benedicto.
“Sawa! Hakuna tatizo!”
Hilo ndilo walilokuwa wamekubaliana, ilikuwa ni lazima Irakoze aanze kusomea utawa ndani ya chuo hicho alichokuwa akifanya kazi kama mpishi. Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu tayari alikwishafanya kazi hiyo kwa miaka mitatu, akachukuliwa na kuanza masomo moja kwa moja.
Kila siku alikuwa akiamka asubuhi na mapema kama wanachuo wengine na kisha kuelekea kanisani ambapo walisali kisha kujiandaa na masomo kama kawaida. Japokuwa hakuwa amesoma sana kipindi cha nyuma lakini uwezo wake wa kawaida ulitosha kabisa kuonyesha kwamba kama angeendelea zaidi basi angeweza kufanikiwa sana katika maisha yake.
Aliishi kama mtumishi wa Mungu, kila wakati alikuwa mtu wa kusali huku rozali ikiwa shingoni mwake. Kila mtu alimheshimu na alipoonekana kwamba yeye ndiye alikuwa mcha Mungu mkubwa kuliko wengine, wakampa uongozi wa bweni pasipo kujua kwamba mwanamke huyo alikuwa na mtoto ambaye alikuwa akisoma nchini Marekani.
Padri Benedicto hakuacha, kwa kuwa katika kila hatua aliyokuwa akipitia Irakoze ilikuwa chini yake, hivyo alihakikisha kwamba hata kwenda nje ya chuo hicho linakuwa jambo jepesi ili mradi mwisho wa siku aweze kuonana naye na kufanya mambo yao.
Alichokifanya ni kukaa chumbani na kuandika barua, alikuwa akiuandikia uongozi wa chuo hicho kwamba kutokana na heshima aliyokuwa nayo Irakoze, aliruhusiwa kila Jumapili kwenda kusali nje ya chuo hicho.
Nafasi hiyo haikutolewa mara kwa mara, ilitolewa mara chache sana tena kwa wanachuo walioonekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Kwa Irakoze hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa na wasiwasi, jinsi nidhamu yake ilivyokuwa chuoni hapo, ilimfanya kila mmoja kukubaliana na padri Benedicto kutokana na jinsi alivyokuwa chuoni hapo.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi nyingine na waliitumia vilivyo kuwa pamoja. Kila kitu kilichokuwa kikifanyika kiliendelea kuwa siri kubwa. Baada ya miaka miwili kukatika, hatimaye aliyekuwa Kardinari wa Kanisa la Kiroma nchini Tanzania, Paulo Alonso akafariki dunia na hatimaye barua kuandikwa kutoka Vatican kwamba Padri Benedicto alitakiwa kutawazwa na kuchukua nafasi hiyo kwani kwa sifa zote za kuwa kardinari alikuwa nazo.
“Lakini kwa nini apewe padri? Kwa nini asipewe askofu?” maaskofu waliulizana tu.
“Hata sisi hatufahamu, ila kwa sababu ni barua iliyoletwa kutoka Vatican, hatuna budi, acha tukubaliane nayo,” alisema askofu mmoja.
Baada ya wiki mbili, padri Benedicto alitakiwa kuelekea nchini Vatican kwa ajili ya kutawazwa na hatimaye kuwa kardinari mkubwa nchini Tanzania. Hiyo ilikuwa nafasi yake pekee, moyo wake ulikuwa na furaha kubwa, hakukuwa na kitu kilichowahi kumpa furaha maishani mwake kama kipindi hicho.
Suala la kuwa na mtoto liliendelea kuwa siri yake, hakutaka mtu yeyote afahamu na alikuwa akijitahidi kufanya kila liwezekanalo kusiwe na mtu yeyote anayelifahamu hilo. Kwenye kila mwaka, alikuwa akimtumia mtoto wake Annabel kiasi cha fedha kwa kutumia akaunti nyingine kabisa iliyosomeka kwa jina la Andrew McDonald, raia kutoka nchini Kenya.
Japokuwa Annabel katika kipindi hicho alikuwa na miaka kumi, lakini aliendelea kufichwa kwamba baba yake alikuwa padri ambaye katika kipindi hicho alitarajiwa kutawazwa na kuwa kardinari nchini Tanzania.
“Unataka kuwa nani ukikua?” aliuliza Benedicto.
“Nataka kuwa mwanasheria.”
“Kwa nini usiwe sista?”
“Sitaki! Nitataka niolewe. Nimesikia kwamba sista haolewi! Kweli baba?”
“Ndiyo!”
“Basi mimi nataka kuwa mwanasheria, ninataka kuolewa baadaye!”
Alikuwa akizungumza na binti yake katika kipindi alichokwenda kumtembelea nchini Marekani. Japokuwa alikuwa nchi nyingine lakini kofia aliyokuwa ameivaa haikutoka kichwani mwake. Shule hiyo aliyompeleka binti yake kusoma ilimtunza vizuri, alipata malezi yote na hakukuwa na shida sana kwa kuwa mara kwa mara alikuwa akifika hapo na kumuona.
Annabel alikuwa binti mzuri, mwenye sifa zote za kuitwa mrembo. Alichanganyikana, alikuwa na sura ya baba yake lakini pia alikuwa na sura ya mama yake. Watu wengi waliokuwa wakimuona, walikiri kwamba binti huyo angekuja kutikisa sana siku za usoni kutokana na urembo wake huo.
“Baba!”
“Naam!”
“Unafanya kazi gani?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Kwani sijawahi kukwambia binti yangu?”
“Hapana! Hukuniambia!”
“Mimi ni mfanyabiashara binti yangu, huwa nasafirisafiri sana,” alijibu Benedicto.
“Kweli baba?”
“Ndiyo! Nikitoka hapa, nakwenda Dubai, nikuletee zawazi gani nikija?”
“Chochote upendacho baba, nitafurahi!” alisema Annabel.
Benedicto hakuwa na jinsi, ni kweli alimpenda binti yake lakini kulikuwa na vitu ambavyo hakutakiwa kuwa mkweli kabisa, alimdanganya kwamba alikuwa mfanyabishara kwa kuwa hakutaka ajue kwamba alikuwa padri ambaye hakutakiwa kuoa au kuwa na mtoto yeyote yule.
Kwake, bado lile liliendelea kuwa siri kubwa, kila siku lilimuumiza moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi, alikubaliana na kila kitu kilichokuwa kiiendelea, na hata kama alifanya dhambi, aliamini kwamba hakukuwa na mwanadamu aliyekuwa mkamilifu mbele za Mungu.
Baada ya siku tatu, akarudi nchini Tanzania ambapo moja kwa moja akawasiliana na Irakoze na kumwambia kuhusu mtoto wao na ndoto aliyotaka kuwa nayo katika maisha yake.
“Kakataa kuwa sista?”
“Amekataa!”
“Daaah! Ngoja niende, nitazungumza naye,” alisema Irakoze.
“Hakuna tatizo!”
Japokuwa aliamini kwamba binti yake angeweza kumsikiliza na hatimaye kukubaliana nao kuwa sista lakini hilo halikuwezekana, bado msimamo wa Annabel ulikuwa ni kuwa mwanasheria mkubwa duniani.
Hakukuwa na mtu aliyemzuia, waliachana naye, aendelee na maisha yake na mwisho wa siku kukamilisha kile alichokuwa akikitaka.
Wakati Annabel akifikisha miaka kumi na sita, alionekana kuwa binti mrembo mno, kipindi kirefu cha maisha yake alikitumia nchini Marekani, hakuwahi kurudi nchini Tanzania, aliondoka huko miaka mingi iliyopita, tangu alipokuwa na miaka minne.
Hakufahamu sehemu yoyote nchini Tanzania, hakufahamu mitaa na hata watu wa huko walikuwa na utamaduni gani. Baada ya kufikisha miaka hiyo, hakutaka kukaa nchini Marekani, alitaka kuwa na muda wa kurudi nchini Tanzania ili aweze kukaa na wazazi wake ambao hakuwahi kukaa nao hata siku moja.
Alitaka malezi yao, alichokifanya ni kuwasiliana nao, hawakuwa najinsi, wakajipanga kwamba mara binti yao atakapofika nchini Tanzania, wampelekea katika nyumba yao nyingine iliyokuwa Kisarawe, pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo waliamini kwamba hakukuwa na watu wengi.
Siku ya safari ilipofika, Annabel akaingia ndani ya ndege tayari kwa kurudi nchini Tanzania. Hapo Marekani akapanda ndege ya Shirika la Ndege la American Airlines ambayo ilikuwa ikifanya safari mpaka nchini Uingereza, Italia na baadaye kuelekea Uholanzi ambapo huko wangebadilisha ndege na kuelekea Dubai, kisha India na Kenya jijini Nairobi na kuingia nchini Tanzania kabla ya kuelekea Afrika Kusini.
Baada ya abiria kutakiwa kuingia ndani ya ndege hiyo, Annabel akasimama na kuanza kuelekea ndani ya ndege hiyo. Kwa muonekano, alionekana kuwa binti mkubwa, mrembo, mwenye mvuto ambaye alivutia sana, kila mwanaume aliyemwangalia, alitamani kuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa.
Wakati ameingia ndani ya ndege hiyo na kukaa katika viti vya watu wawili, akaja mwanaume mmoja, alionekana kuwa kijana mtanashati, aliyependeza, alivalia suti ya gharama, muda wote uso wake ulionekana kuwa na tabasamu pana, alimuona Annabel, tabasamu likaongezeka usoni mwake.
“How are you cute,” (Habari yako, mrembo) alimsalimia Annabel.
“I’m fine, you are welcome,” (Salama, karibu) alimkaribisha mwanaume yule aliyejitambulisha kwa jina la Ethan Dylan.

INAENDELEA...                        

HADITHI!!!!! HADITHI SEHEMU YA TANO

BIASHARA YA KIFO
sehemu ya 05

Kwa kumwangalia usoni tu, padri Benedicto alionekana kuhitaji msaada, alitia huruma mno, macho yake alikuwa ameyapeleka usoni mwa Irakoze huku akionekana kuwa na hofu kubwa. Kile alichokuwa amekifanya kilikuwa ni kinyume na sheria za kanisa hilo hivyo kama kanisa lingejua kile kilichokuwa kimetokea, lingekuwa tatizo kubwa.
Hakukuwa na mtu ambaye angeweza kumsaidia katika kipindi hicho zaidi ya msichana huyo. Alizungumza naye kwa kipindi kirefu, tena kwa unyenyekevu mkubwa na mwisho wa siku akamwambia ukweli kwamba alitakiwa kuondoka mahali hapo.
“Niende wapi?”
“Popote pale, ili mradi utoke ndani ya nyumba hii,” alisema padri Benedicto.
“Kwa hiyo unanifukuza?”
“Hapana! Sikufukuzi.”
“Ila?”
“Nitakupangia chumba, utakwenda kuishi huko mpaka utakapojifungua, nakuahidi kukusaidia kwa kila kitu,” alisema padri Benedicto.
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Hicho ndicho walichokubaliana, padri hakutaka Irakoze abaki nyumbani hapo kwa kuhofia kwamba watu wangeweza kujua kwamba alikuwa mjauzito na hivyo mwisho wa siku kumletea matatizo, alichokifanya ni kumwambia aondoke nyumbani hapo huku akimgawia kiasi cha shilingi milioni moja.
Kabla ya kuondoka kwanza akaanza kutafuta chumba ambacho alikipata maeneo ya Sinza Makaburini, huko ndipo alipoanza maisha yake. Alikuwa akihudumiwa kila kitu na padri huyo, kuanzia chakula, mavazi, vitu vya ndani na mambo mengine mengi.
Alipewa kiasi cha shilingi milioni moja kila mwezi kitu kilichompeleka kuanza kufanya biashara zake binafsi, japokuwa zilikuwa ndogondogo lakini akafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyaendesha maisha yake.
Katika kipindi hicho cha kwanza tumbo lake halikuwa likionekana lakini baada ya miezi kadhaa kupita, kila mtu aliyekuwa akimwangalia alijua kwamba msichana huyo alikuwa mjauzito.
Padri Benedicto akawa akifika sana nyumbani hapo nyakati za usiku tena huku akiwa amevalia kofia kubwa ili asiweze kujulikana. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kilikuwa siri kubwa mno kiasi kwamba hakukuwa na mtu aliyefahamu ukweli.
Baada ya miezi tisa kukatika, hatimaye Irakoze akajifungua mtoto wa kike aliyempa jina la Annabel kama ambavyo padri Benedicto alivyotaka aitwe na hivyo maisha yake na mtoto wake kuanza.
Padri huyo hakukata mguu nyumbani hapo, kila alipomuona Annabel, moyoni mwake alijisikia furaha mno, hakuamini kama mwisho wa siku na yeye alifanikiwa na kuitwa baba. Moyoni mwake alijiona kuwa mwanaume wa shoka, alijikubali japokuwa sheria ya kidini ilimkataza kuwa na mwanamke yeyote, kuona au kuzaa mtoto.
Siku zaikaendelea kukatika, hakuacha kufika nyumbani hapo, aliendelea kumlea Irakoze na mtoto wake na baada ya miaka mitatu kupita huku akiwa amekwishaanza kumjengea nyumba Irakoze maeneo ya Mbezi Beach, hapo ndipo alipoamua kumwanzisha Annabel Shule ya Chekechea ya Antonino iliyokuwa Mbezi Beach ambapo wanafunzi wengi walisoma shuleni hapo walikuwa ni wale waliotoka katika familia za kitajiri.
Mwaka uliofuata ambapo Annabel aliingia mwaka wa nne hapo ndipo alipoanza kumsumbua mama yake kuhusu baba yake. Kila siku alikuwa mtoto wa kulia tu, hakukuwa na kitu alichokuwa akikitamani wakati huo kama kumuona baba yake tu.
“Mama nataka kumuona baba.....” alisema Annabel kwa sauti ya chini huku akilia.
“Baba yako atakuja.”
“Lini?”
“Kesho! Twende shule kwanza.”
“Sitaki kwenda mpaka nimuone baba.”
“Atakuja tu mwanangu! Twende shule kwanza.”
Japokuwa aligoma kwenda shule lakini Irakoze hakuwa na jinsi, alimlazimisha Annabel mpaka akakubali kwenda shuleni. Njiani, alikuwa akilia tu, hakunyamaza, kila walipofika bado alikuwa akilia kumuona baba yake.
Hicho kilimuumiza sana Irakoze, kila aliposikia kwamba binti yae mzuri akimuulizia baba yake, moyo wake ulimuuma mno. Hakuwa na jinsi, alimpigia simu padri Benedicto na kumwambia ukweli kwamba binti yake alitaka kumuona, hivyo alitakiwa kufanya kila awezalo aje kumuona.
“Nitakuja.”
“Lini?”
“Sijajua! Ila nitakuja hivi karibuni.”
“Unajua mtoto wako anasumbua sana, siku hizi hata kula hataki!”
“Kisa?”
“Anataka kukuona wewe!”
“Aiseee! Nitakuja basi.”
“Lini?”
“Kesho usiku!”
“Sawa!”
Siku iliyofuata usiku, padri Benedisto alikuwa mahali hapo, kitu cha kwanza kabisa alitaka kumuona binti yake. Japokuwa mara kwa mara alikuwa akifika na kumuona lakini siku hiyo Irakoze akaamua kumwambia Annabel kwamba yule alikuwa baba yake.
Annabel akafuata na kumkumbatia, alionekana kuwa na furaha sana na hakutaka kutoka mikononi mwa baba yake. Kila alipomwangalia binti yake, alifanana naye sana, alijifariji sana, japokuwa sheria hazikutana padri kuwa na mtoto lakini kwake ilionekana kuwa furaha kubwa. 
Kuanzia siku hiyo, mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani hapo huku akimkataza Irakoze asimwambie Annabel kama alikuwa padri kuepuka matatizo hapo baadae. Hilo wala halikuwa tatizo, Irakoze akakubaliana naye kwamba jambo hilo liendelee kuwa siri siku zote.

“I will kill you, bullshit,” (Nitakuua kinyesi cha ng’ombe)
“Do you really want to kill me?” (Unataka kuniua?)
“Yes!” (Ndiyo!)
“Ok! Just shoot me.” (Sawa! Nipige risasi)
“I will kill you.” (Nitakuua)
“Shoot me! Shoot me right here,” (Nipige risasi, nipige hapa)
Lilikuwa kundi kubwa la watu zaidi ya thelathini waliozunguka sehemu iliyokuwa na mapipa makubwa ya uchafu katika mtaa wa kimasikini wa Manhattan uliokuwa katika Jiji la New York nchini Marekani.
Kila mtu alikuwa akimwangalia kijana aliyeshika bunduki, alikuwa amemnyooshea mwanaume mmoja, alionekana kuwa mtu mzima, alikuwa akitamka maneno kwamba angempiga na risasi endapo tu angeendelea kuzungumza naye mahali hapo.
Kijana huyo aliyeonekana kuchoka kimaisha aliitwa Ethan Dylan, alikuwa kijana mwenye asili ya Kingereza ambaye aliishi nchini Marekani. Katika maisha yake yote, hakuwahi kumuona baba yake, kipindi ambacho mama yake aliondoka nchini Marekani na kwenda Uingereza ndipo alipokutana na baba yake, akarudi nchini mwao Marekani ambapo huko ndipo alipokutana na mwanaume aliyeitwa George.
Wawili hao wakapenda na kuoana. George alikuwa mwanaume mpole, aliyejiheshimu ambaye kila siku alitamani sana kumuona Ethan akikulia katika maisha mazuri, yenye heshima ambayo yangemfanya kuwa baba bora miaka ya baadae.
Kutokana na eneo walilokuwa wakiishi kuwa na vijana wengi wenye fujo, waliojihusisha na madawa ya kulevya, naye Ethan akajikuta akiingia katika huo mkumbo na mwisho wa siku kuwa mhuni wa mtaani.
Mama yake aliumia sana lakini hakuwa na cha kufanya. Kama kuongea, aliongea sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika. Baadaye akajiingiza kwenye makundi ya wahuni, huko akaanza kuuza madawa ya kulevya na mwisho wa siku kumiliki bunduki yake.
Siku hiyo ambayo alizungukwa na watu wengi, alikuwa amemnyooshea bunduki baba yake wa kambo, mzee George. Alimwambia ukweli kwamba alitaka kumpiga risasi. Maneno hayo hayakumshangaza mzee huyo, alichokifanya ni kumsogelea Ethan na kuiweka bunduki ile kwenye paji lake la uso na kumwambia ampige risasi hapohapo.
“Shoot me right here,” (Nipige risasi hapa) alisema mzee George, watu wote waliokuwa wamewazunguka walianza kuogopa kwani walimjua fika Ethan, hakuwa kijana mwenye masihara, alipokuwa akishinda bastola, hakurudisha nyuma hata mara moja, alikuwa tayari kuua, pasipo kutegemea, akaikoki bastola yake kitendo kilichomfanya kila mtu kushtuka mahali hapo. Hata mzee George naye kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Ethan alionekana kukasirika mno, hata mwili wake ulimtetemeka.


INAENDELEA...

Tuesday, 23 January 2018

HADITHI!!!......SEHEMU YA NNE

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 04

Hakukuwa na kitu alichokifikiria zaidi ya ngono, alitaka kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza katika maisha yake, hakutaka kumuacha Irakoze hivihivi, alitaka kuhakikisha kwamba kibaridi kile kilichokuwa kikipiga, ni lazima kikatishwe na joto la mwili wa Irakoze.
Alitembea kwa harakaharaka kama mtu aliyekuwa akiwahi kitu fulani, alipofika ndani, akasikia maji yakimwagika bafuni, akajua ni lazima Irakoze alikuwa ndani ya bafu lile akioga. Hakutaka kujiuliza, akausukuma mlango, ukafunguka, naye akazama ndani.
“Aaaah! Padri!” alisema Irakoze huku akijifanya kujificha.
“Usiogope.”
“Naoga padri, naomba uende nje,” alisema Irakoze.
Hiyo ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa acheze, padri Benedicto hakutaka kutoka, alichokifanya ni kuusukuma mlango na kubaki humohumo. Kwa sababu naye mwenyewe alikuwa akimpenda sana padri huyo kutokana na uzuri wa sura yake, hakutaka kuiacha nafasi hiyo, akaitumia vilivyo na hivyo kujikuta wakigusana miili yao, maji ya bomba la mvua yaliwamwagikia, walipapasana hapa na pale na hatimaye kufanya dhambi.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kila kitu, mchezo walioufanya siku hiyo ukampelekea hata Irakoze kuhama chumba chake na kuhamia kwa padri huyo. Waliishi kama mume na mke, hakukuwa na mtu yeyote nje ya nyumba hiyo aliyefahamu kile kilichokuwa kikiendelea.
Ilikuwa siri kubwa mno, na kila alipotoka nyumbani, padri Benedicto alijifanya kuwa mtakatifu mno, kumbe jana yake tu alikuwa amelala na Irakoze usiku mzima. 
“Tumsifu Yesu Kristo!” alisema padri yule.
“Milele Amina.”
Usiri mkubwa uliendelea, padri Benedicto hakutaka kuonekana kuwa rahisi kwa wanawake wengine ambao walimfuata kwa kisingizio cha kutaka kumwagiwa maji ya baraka kumbe upande wa pili walikuwa wakihitaji kulala naye.
Mwanamke aliyekuwa naye nyumbani, alimtosheleza na hata alipokuwa akifuatiliwa na wanawake wengine, hakutaka kuwakubalia kwa kisingizio kwamba alikuwa mtu wa Mungu na hakutakiwa kuoa kutokana na cheo alichokuwa nacho.
“Ninakupenda mpenzi,” alisema Irakoze.
“Nakupenda pia!”
“Hivi siku ikitokea nikapata mimba?”
“Utapataje? Haiwezekani, tupo makini kila siku, wala usijali, mimba haiwezi kutokea,” alisema padri Benedicto.
Hakukuwa na aliyejali sana, padri Benedicto alikuwa na uhakika kwamba kila kitu ambacho kiliendelea kamwe asingeweza kumpa mimba msichana huyo. Siri kubwa iliendelea, waliishi kama mume na mke.
Wakati mwingine padri Benedicto hakuwa akielekea kanisani, alibaki nyumbani kwa ajili ya kufanya mapenzi na msichana huyo tu. Japokuwa kila siku washirika walimtembelea padri wao lakini hakukuwa na yeyote aliyefahamu kama watu hao walikuwa kwenye uhusiano mkubwa wa kimapenzi.
Siku zikakatika, miezi ikaendelea kukatika. Padri Benedicto akaingia moja kwa moja kwenye ulimwengu wa kishetani, naye akaanza kwenda klabu usiku, akaanza kunywa pombe kali zilizomfanya hata kutokuthamini kazi yake ya upadri.
Mabadiliko yale yalimshangaza mno Irakoze, hakutaka kuzungumza naye sana kwa kuamini kwamba mabadiliko hayo yangetokea kipindi hicho tu, cha kushangaza, hakuacha, kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyozidi kubadilika.
Kila siku usiku, akawa mtu wa kutoka na kwenda klabu, huko, alikuwa akivalia kofia kubwa ili asijulikane na mtu yeyote. Alikunywa pombe na wakati mwingine kulewa mno, maisha ya kidunia yakaanza kumteka kiasi kwamba wakati mwingine alipokuwa akirudi nyumbani na kulewa, kesho yake hakwenda kabisa kanisani kwani kichwa bado kilikuwa na pombe kali.
“Kuna kitu ninataka kuzungumza nawe,” alisema Irakoze.
“Kitu gani?”
“Mbona sikuelewielewi! Hebu tulia kwanza,” alisema msichana huyo.
“Nitulie kivipi tena? Unajua leo lini?”
“Jumapili!”
“Basi subiri kwanza niende kanisani,” alisema padri Benedicto.
Japokuwa Irakoze alikuwa na jambo muhimu la kuzungumza na padri huyo lakini hakuweza kupata nafasi hiyo. Ilikuwa ni Jumapili ya tatu tangu asitishe kwenda kanisani kwa kisingizio cha kuwa bize kufuatilia mizigo iliyotumwa kutoka nchini Vatican kwa maendeleo ya kanisa hilo.
Ingawa alikuwa akidanganya kwa kujifanya mfuatiliaji namba moja lakini hakukuwa na mtu aliyemshtukia kwamba ni pombe za janausiku ndizo zilizomuweka nyumbani na kushindwa kabisa kwenda kanisani.
Siku hiyo alipanga kwenda huko kwa ajili ya kuhubiri, alijua ni kwa jinsi gani washirika wake walikuwa wamemkumbuka kwani katika kipindi chote alichokuwa akikaa nyumbani, alikuwa akipigiwa simu na kuuliziwa maendeleo yake.
Siku hiyo alipoonekana kanisani, kila mshirika alikuwa na furaha, wiki tatu ambazo hakuonekana kabisani hapo zilionyesha kila dalili kwamba kanisa hilo lingepwaya sana na hatimaye lingeweza kupotea kabisa.
Ujio wake ukaibua ari ya washirika wake na hatimaye kuendelea na huduma kama kawaida. Kwa kumwangalia, usingeweza kuamini kwamba jana usiku alishinda klabu ya muziki, alionekana mchangamfu na hata macho yake hayakuonyesha kabisa kama alikuwa mtu aliyekesha.
Japokuwa alikuwa akihubiri na kuwabariki watu waliokuja na watoto wao kanisani hapo lakini mara alipokumbuka kwamba Irakoze alitaka kuzungumza naye asubuhi ya siku hiyo, ghafla amani ikakatika.
Hakukuwa na kitu alichokiogopa kama kuambiwa kwamba mtu fulani alitaka kuzungumza naye. Hakujua ni kitu gani kiliendelea lakini mwisho wa siku akataka kukaa chini na msichana huyo ili kumsikia alikuwa na jambo lipi la kuzungumza.
Ibada ilipokwisha, hakutaka kukaa kanisani na kuwasalimia washirika, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea nyumbani kwake. Alipofika huko, kama ilivyokuwa siku nyingine, alipokelewa kwa mahaba mazito mpaka chumbani, hata kabla hajafanya lolote, akavuliwa joho na kupigwa mabusu mfululizo, ndani ya dakika tatu tu, alibaki kama alivyozaliwa.
Kilichofuata ni kilekile kilichokuwa kikitokea siku zote, walifanya dhambi kwa takribani masaa matatu na ndipo kila mmoja akaridhika na kutulia pembeni ya mwenzake.
“Aya niambie ulitaka kuniambia nini asubuhi,” alisema padri Benedicto.
“Una moyo?”
“Ninao. Hebu niambie wala usinitishe.”
“Usiogope, nafikiri ni baraka kutoka kwa Mungu.”
“Ipi?”
“Nina mimba yako!”
“Unasemaje?” aliuliza padri huku akionekana kushtuka.
“Nina mimba yako!”
Padri Benedicto akasimama na kuanza kumwangalia Irakoze, hakuamini kile kilichokuwa kimeongelewa maahali hapo, alimwangalia msichana yule, ndiyo kwanza alikuwa akitabasamu kwa furaha, hakuonekana kujua ni kwa jinsi gani padri alijisikia moyoni mwake.
Kama masharti ya kanisa hilo, hawakutakiwa kuoa, si kuoa tu, hawakutakiwa kuwa na mtoto pia. Kauli ya Irakoze ilimuweka katika wakati mgumu,  mwili wake ukaanza kutetemekea huku kijasho chembamba kikimtoka.
“Unasemaje?”
“Nina mimba yako!”
Alitamani jibu libadilike na kuambiwa kwamba alikuwa akitaniwa, kile alichoambiwa sekunde chache ziliopita kilikuwa kilekile alichoambiwa kwa mara nyigine tena, akajikuta akitoka chumbani humo na kuelekea sebuleni.
“Kuna nini?” aliuliza Irakoze.
“Hivi unajua misingi ya kania letu?”
“Ndiyo! Ila mtoto ni baraka mpenzi!”
“Haiwezekani! Mtoto si baraka katika maisha yangu! “
Hakukuwa na kitu kilichomchanganya katika maisha yake kama hicho, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwamba baada ya kufanya sana mapenzi mwisho wa siku msichana wake alikuwa mjauzito.
Wakati mwingine alifikiria kuikataa mimba hiyo ila kila alipona kwamba ndipo kungekuwa na madhara zaidi kwa msichana huyo kutangaza, akaogopa. Kama ilivyokuwa siri katika kipindi cha nyuma, ilitakiwa kuendelea kuwa siri maisha yake yote, iwe isiwe, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba jambo hilo halijulikani na mtu yeyote yule.
“Naomba tufanye kitu ili unifiche na aibu hii,” alisema Padri Benedicto huku kijasho chembamba kikianza kumtoka na mwili ukizidi kumtetemeka. Irakoze akamkazia macho.


INAENDELEA...

HADITHI!!!!!.....SEHEMU YA TATU

BIASHARA YA KIFO
sehemu ya 03


Alijulikana kwa jina la Pius Massawe, Mchaga kutoka mkoani Kilimanjaro, alikuwa kijana mwenye sura nzuri kiasi kwamba wanawake wengi wakatokea kumpenda kutokana na uzuri wa sura aliokuwa nao.
Wasichana wengi kutoka katika Shule ya Sekondari ya Majengo mkoani humo walivutiwa na Pius lakini kijana huyo hakutaka kabisa kujihusisha na mambo ya mapenzi kabisa. Wasichana hao hawakutaka kuvumilia, waliamua kumfuata na kumwambia ukweli kwamba walikuwa wakimpenda lakini Pius hakutaka kukubaliana nao, aliwakataa kitu kilichowafanya watu wengi kumshangaa.
Uvumi ukaanza kusikika kwamba Pius alikuwa akishiriki mapenzi ya jinsia moja, uvumi huo ulivuma kwa kasi lakini yeye mwenyewe hakutaka kulizungumzia suala hilo, alijua kwamba kulikuwa na maneno mengi yangesemwa, kwake, hizo zote alizichukulia kama changamoto.
Mbali na uzuri wa sura aliokuwa nao, Pius alikuwa na uwezo mkubwa darasani, katika kila mtihani, alikuwa akiongoza kitu kilichowachanganya watu wengi kabla ya kugundua kwamba mtu huyo alikuwa na akili za kuzaliwa, yaani kile alichokuwa akifundishwa leo, hakuweza kukisahau hata kama ni miaka mingapi ingepita.
Wanawafunzi wengi walikimbilia kwake kufundishwa, Pius hakuwa na maringo, alimfundisha kila mtu japokuwa wanawake wengi walitumia njia hiyo kumtongoza lakini bado msimamo wake ulibaki kuwa uleule kwamba asingeweza kutembea na msichana yeyote yule shuleni hapo.
“Kwani tatizo nini Pius?” aliuliza msichana Thedosia, japokuwa alisifika kwa uzuri shuleni hapo kwa upande wa wanawake, lakini kwa Pius alionekana si chochote.
“Ninataka kuwa padri.”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Kwa hiyo hautooa?”
“Hakuna tatizo. Siwezi kufanya mapenzi na msichana yeyote,” alisema Pius huku akimwangalia msichana huyo usoni.
Huo ndiyo ulikuwa msimamo wake, hakutaka kufanya mapenzi na msichana yeyote yule. Pius alikuwa kijana wa tofauti na wengine, alihusudu sana ibada, kila siku alipokuwa akihitajika kwenda kanisani, alikwenda, alipofika huko, alikaa katika kiti cha mbele kabisa na kuanza kusali.
Kila alipokuwa, rozali ilikuwa mkononi mwake, na kama haikuwa mkononi, aliichukua na kuivaa shingoni. Alikuwa hivyo, nyumbani napo kulikuwa kama shuleni. Uzuri wa sura yake ulizidi kuwatetemesha wanawake wengi, wengine walijipendeza waziwazi lakini hakuwa na habari nao, alichokuwa akikihitaji ni kuwa padri tu.
Alipomaliza kidato cha nne na kujiunga na cha tano katika Shule ya Sekondari ya Tambaza iliyokuwa jijini Dar es Salaam. Kila alipofika, Pius alikuwa gumzo, japokuwa alipokuwa mkoani Kilimanjaro aliambiwa kwamba atakapofika Dar es Salaam basi msimamo wake ungeweza kulegea lakini huko akawa vilevile kiasi kwamba watu wakampa jina la padri kitu kilichomfurahisha mno.
Alipomaliza kidato cha sita kwa masomo ya kawaida, akafaulu lakini akajiunga na chuo cha upadri kilichokuwa Morogoro na kisha kuanza masomo rasmi. Haikuwa kazi ngumu, alizingatia masomo yake, kila siku asubuhi alikuwa akiamka na wenzake na kwenda kanisani kusali, walipomaliza na ndipo walipoendelea na mambo mengine.
Alisoma huko kwa muda wa miaka mitatu na ndipo walipoandaliwa kwenda kumalizia masomo ya mwisho katika Jiji la Venice nchini Italia. Ilikuwa furaha kwake kwani alibakiza hatua chache kabla ya kufika pale alipotaka kufika.
Kutoka Venice mpaka Vatican haikuwa mbali sana, mara kwa mara alikuwa akielekea huko na kukutana na viongozi wa dini ya Kiroma na kuzungumza nao mawilimatatu kitu kilichomfanya kujisikia vizuri na kuahidi kushinda kile kilichobakia mbele yake.
Huko ndipo alipopewa jina la Benedicto badala la lile la Pius alilokuwa akilitumia kabla. Baada ya kukaa huko Venice kwa miaka miwili ndipo aliporudi nchini Tanzania na kupewa kanisa huku akijulikana kwa jina la Padri Benedicto.
Kanisa likajaza wanawake wengi kuliko wanaume, tetesi zilizokuwa zikisikika kwamba kanisa hilo lilikuwa na padri aliyekuwa na sura nzuri iliwachanganya wanawake wengi na hivyo kutaka kwenda huko kushuhudia kwa macho yao.
Walipomuona, waliamini kwamba duniani kulikuwa na wanaume wenye sura nzuri mno, kila walipomwangalia padri wao, walimtamani mno.
“Jamani hii sheria ya mapadri kuoa si ipitishwe tu, nahisi kama bahati inaweza kuniangukia,” alisikika akisema msichana mmoja.
“Bahati ya nini?”
“Kuolewa na padri Benedicto, ninampenda sana jamani!”
“Wewe Upendo, humuogopi Mungu!”
“Namuogopa, lakini kwa nini ameamua kutupa jaribu kubwa namna hii?”
Padri Benedicto alikuwa akiishi peke yake nyumbani kwake, wafanyakzi wengi wa ndani aliokuwa akiwahitaji walikuwa wa kiume tu ambao wengi alikorofishana nao na mwisho wa siku kuwafukuza kihekima.
Baada ya kufukuza wafanyakazi watano, akaamua kuishi peke yake, hakutaka tena kuwa na mfanyakazi yeyote nyumbani kwake kwani aliona kama angeweza kufanya kazi peke yake pasipo mfanyakazi yeyote yule.
“Ila kuna msichana ana matatizo sana, naomba aje akusaidie padri,” alisema mama John, mwanamke aliyekuwa ameonana na Irakoze.
“Nimsaidie vipi?”
“Aje kufanya kazi hapa!”
“Msichana?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Haiwezekani hata kidogo.”
Japokuwa padri Benedicto alikataa lakini mama John hakuacha kumbembeleza akubaliane naye kwani mtu kama yeye alihitaji mfanyakazi wa kike kwa ajili ya kufanya usafi wa nyumba muda wote kitu ambacho kwa kiasi fulani kikaanza kumuingia padri huyo.
Mbali na kumwambia hivyo, pia alimsimulia historia ya kusikitisha ya msichana Irakoze kiasi kwamba padri akaingiwa na huruma na kuona kwamba kumsaidia msichana huyo ilikuwa kama baraka kwa Mungu kwa kuwa ameamua kumtoa mtu fulani kutoka sehemu moja ya chini na kumuweka sehemu ya juu.
Wakakubaliana na hivyo mama John kuelekea nyumbani ambapo akamchukua Irakoze na kuelekea naye nyumbani hapo. 
“Ni mzuri mno, sijawahi kuona mwanaume mzuri kama huyu,” alijisemea Irakoze katika kipindi alichomuona padri Benedicto kwa mara ya kwanza.
Hiyo ndiyo ikawa siku ya kwanza kukutana kwa watu hao, Irakoze akaanza kazi ndani ya nyumba hiyo. Alikuwa msichana mwenye heshima kubwa, kila siku alikuwa mtu wa kuvaa mavazi marefu ambayo aliamini kwamba yasingemtia majaribu padri huyo.
Waliheshimiana mno, kila siku asubuhi walikutana sebuleni, walishikana mikono na kuanza kusali kisha kuendelea na ratiba nyingine. Katika kipindi chote hicho, Irakoze alikuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa padri huyo, alitamani kumwambia ukweli kwamba alimpenda lakini aliogopa kufanya hivyo, akabaki akiugulia moyoni mwake tu.
Siku zikaendelea kukatika, heshima ilikuwa kubwa ndani ya nyumba, Irakoze aliendelea kufanya kazi ndani ya nyumba hiyo huku kila siku akijitoa kitendo kilichomfurahisha padri Benedicto kiasi kwamba alijiona kuchelewa mpaka kuchukua uamuzi wa kumuajiri mfanyakazi wa kike.
“Nakuja, niandalie chakula,” alisema padri Benedicto.
Siku hiyo hakuwepo nyumbani, alikuwa kanisani akiendelea na huduma, mawingu mazito yalitanda angani kuonyesha kwamba muda wowote ule mvua ingeweza kunyesha. Mara baada ya kumaliza kila kitu likiwa suala la kupika chakula, Irakoze akachukua khanga yake na kuelekea bafuni kuoga.
Alipokuwa huko, akasikia mvua kubwa ikianza kunyesha huku kiubaridi kikianza kuongezeka. Alichokifanya Irakoze, akatoka bafuni na khanga yake kisha kutoa ndoo nje kwa ajili ya kukinga maji ya mvua yaliyokuwa yakidondoka.
Mwili wake ukalowa, khanga ikanata mwilini mwake, umbo lake lenye mvuto, makalio yaliojaajaa yakawa yanaonekana vizuri kabisa. Hakuwa na wasiwasi wowote ule, alikuwa peke yake nyumbani hapo hivyo aliendelea kufanya kazi yake.
Wakati yupo hapo akiendelea kukinga maji, mara geti likafunguliwa na padri Benedicto kuingia. Irakoze hakumuona padri huyo, aliendelea kukinga maji huku wakati mwingine akijimwagia, kifua chake kikanata kwenye ile khanga, kila kitu mwilini mwake kilionekana wazi.
Padri Benedicto alipoona hivyo, moyo wake ukashtuka, hakupiga hatua, alibaki akimwangalia Irakoze huku akiwa na mwamvuli wake. Alibaki akimeza mate na maeneo ya zipu yake kuanza kusogea mbele. Alichanganyikiwa, kila alipojitahidi kuyaamisha macho yake, yaligoma kabisa kuhama.
Mpaka Irakoze anageuka na kumwangalia padri huyo, alikuwa hoi, kwa kujishtukia, Irakoze akamsalimia na kisha kuelekea ndani, sehemu ya nyuma ilikuwa ikichezacheza, padri akaona haiwezkani, japokuwa hakuwahi kulala na mwanamke yeyote maishani mwake, uzalendo ukamshinda, pepo la ngono likamwingia, mwili wake ukaanza kumsismka huku akihisi vijidudu fulani vikianza kumtembelea mwilini mwake, naye akaanza kuelekea ndani huku akiwa amechanganyikiwa kimahaba, pepo la ngono lilishamvaa, hakukubali, alitaka kuonekana kwamba hata na yeye alikuwa mwanaume.


INAENDELEA...                        

Sunday, 21 January 2018

HADITHI!!!!!.........SEHEMU YA PILI

BIASHARA YA KIFO

Sehemu ya 02

Hawakujua kitu kilichokuwa kikiendelea nje, hawakujua kama kundi la wanawake likiongozwa na mama mwenye nyumba liliingia ndani na kukisogelea chumba walichokuwa huku wakiwa wamelaliana kimahaba.
Ghafla, huku wakiwa wametekwa na uwepo wa mahaba mahali hapo, wakashtukia mlango ukifunguliwa na kundi zima la wanawake hao kuingia ndani. Kwanza wakashtuka, wakawaangalia vizuri wanawake wale, alikuwepo mke wake pia.
Mzee Saidi akashtuka, hakuamini kile alichokuwa kikiona, mdomo wake ukawa mzito kusema chochote kile. Mkewe alionekana kuvimba kwa hasira, hakuamini kile alichokuwa akikiona chumbani humo, mume wake ambaye kila siku alikuwa akimuamini ndiye yule aliyekuwa na mwanamke kitandani kwake, tena mfanyakazi wake aliyemtoa kijijini.
Irakoze alivyoona hivyo, akaanza kuomba msamaha huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake. Hata kabla bi Hadija hajazungumza lolote lile, akamvamia msichana huyo wa kazi na kuanza kumpiga.
Kundi lile la wanawake halikugobelezea, lilikuwa likishadadia kile kilichokuwa kikiendelea chumbani pale. Ni mzee Saidi ndiye aliyechukua jukumu la kuanza kuamulia lakini bi Hadija hakushikika, alikuwa akitukana hovyo.
“Wewe malaya kweli unaamua kunichukulia mume wangu, tena unalala naye kitandani kwangu, sasa utanitambua,” alisema bi Hadija huku akimshambulia Irakoze.
“Hadija, hebu muache mtoto wa watu.”
“Unagombelezea? Malaya mkubwa wewe, unagombelezeaaaaa?” 
Ugomvi ulikuwa mkubwa, wanawake wale wengine walikuwa wakizungumza maneno yenye kumuumiza Irakoze juu ya kile alichokuwa amekifanya, kila mmoja alimshutumu huku wengine wakimpiga masingi na kumzomea.
Irakoze aliumizwa kutokana na kipigo alichopewa lakini hakuwa na jinsi, kama maji, tayari yalikwishamwagika na hivyo kufukuzwa nyumbani hapo. Hakutakiwa kukaa, mchana huohuo akafukuzwa na kuondoka nyumbani hapo huku akilia, furushi la nguo zake lilikuwa mikononi mwake.
Alijutia kitendo alichokuwa amekifanya, alianza kujuta kwani kilimuumiza mno. Alipiga hatua kuelekea Magomeni Mikumi ambapo huko akachukua barabara ndogo iliyokuwa ikielekea Mwembe Chai kupitia ilipokuwa nyumba ya marehemu Sheikh Yahya.
Alipofika njiani, mvua kubwa ikaanza kunyesha, hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kwenda kwenye nyumba moja aliyoiona kufaa na kisha kujikinga na mvua ile iliyokuwa ikinyesha mno. Hapo ndipo akachukua muda mwingi kuanza kulia, 
“Nitakwenda wapi mimi? Nitakwenda wapi mimi?” alijiuliza huku akilia.
Mvua ilichukua zaidi ya nusu saa mpaka kuacha kunyesha. Alipoona imeacha, hapo ndipo akalishika furushi la nguo zake na kisha kusonga mbele. Alikuwa akielekea wapi? Hakujua, alihitaji kuondoka mbali na nyumba ya mzee Saidi
 Alikwenda na barabara hiyo mpaka alipokuta njia panda, barabara moja ilikuwa ikielekea Mwembe Chai na nyingine Mburahati, alichokifanya ni kuchukua barabara ya kuelekea Mburahati ambapo aliamini kwamba angeweza kupata msaada wowote ule.
Alisonga mbele, furushi lilikuwa kichwani mwake huku akibubujikwa na machozi. Aliona dunia imemgeukia, hakuwa na pa kukimbilia zaidi ya kwenda mbele kama mtu aliyekuwa akibahatisha sehemu fulani.
Safari yake iliishia nje ya nyumba moja, haikuwa ya kifahari, ilikuwa nyumba ambayo kwa kiasi fulani ilionekana kuchoka. Kulijaa matope lakini hakutaka kujali, kwa kuwa kulikuwa na kibaraza, akaenda na kutulia hapo.
Kumbukumbu za maisha yake zikaanza kujirudia kama mkanda wa filamu kichwani mwake, alikumbuka mengi tangu siku ya kwanza alipofika jijini Dar es Salaam mpaka siku hiyo. Alihuzunika na kujutia uamuzi wake wa kutembea na mzee Saidi, ila pamoja na hayo yote, alitakiwa kupambana kwani alijua kwamba huo usingekuwa mwisho wa maisha yake.
“Habari yako!” ilisikika sauti ya mwanamke mmoja, alikuwa amefika nyumbani hapo huku mkononi akiwa ameshika Biblia.
“Salama! Shikamoo mama!”
“Marahaba binti mzuri, hujambo?”
“Sijambo!”
Baada ya salamu ile, mwanamke yule hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kufungua mlango na kuingia ndani. Irakoze hakutoka kibarazani hapo, aliendelea kukaa huku akionekana kuwa na mawazo mengi.
Mpaka inafika saa kumi na mbili jioni, bado hakujua aende wapi, hakuijua vizuri Dar es Salaam kwani kipindi cha miaka miwili kukaa ndani ya jiji hilo, hakuwa mtembeaji, alikuwa mtu wa kutulia tu nyumbani, akitoka, kaenda gengeni na kurudi nyumbani.


INAENDELEA...

HADITHI!!......... HADITHI.................

BIASHARA YA KIFO
Sehemu ya 01:

Imetungwa na Nyemo Chilongani

Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha, mitaro midogo ikaanza kujaa maji huku baridi likianza kupiga kwa nguvu ndani ya jiji la Dar es Salaam. Waliokuwa ndani ya nyumba zao, wakajifungia huku wale waliokuwa barabarani wakinunua miamvuli kwani mvua ile kubwa haikuonekana kuwa na dalili za kupungua hata mara moja.

Watu wengine walikuwa wakikimbilia sehemu zilizokuwa na uwezo wa kuzuia wasilowanishwe na mvua hiyo, wengine, walikubaliana na kile kilichokuwa kikiendelea hivyo kuendelea na kazi zao au safari zao huku wakiendelea kulowa.
Nje ya nyumba moja kubwa, msichana mrembo, mwenye sura nzuri, aliyekuwa na umbo lenye mvuto ambalo vijana wa sasa wangeliita namba nane alikuwa amesimama huku mkononi mwake akiwa ameshika furushi la nguo lililokuwa na nguo nyingi zilizofungwa kwa khanga.

Pale alipokuwa, macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa na kitu moyoni mwake, hakuonekana kuwa mwenye furaha hata mara moja, baada ya dakika chache, machozi yale yaliyojikusanya machoni mwake yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Msichana huyu aliitwa kwa jina la Irakoze, baba yake alikuwa Mrwanda na mama yake alikuwa Mnyaturu kutoka mkoani Singida. Historia ya maisha yake ilianzia mbali, miaka miwili iliyopita, alikuwa akiishi mkoani Singida ambapo baadaye mwanamke aliyeitwa kwa jina la Hadija aliyetoka jijini Dar es Salaam akafika kijijini kwao na kumchukua kwa lengo la kwenda kufanya kazi katika nyumba yake iliyokuwa Magomeni jijini Dar.

Hilo ndilo lilikuwa lengo lake, aliporuhusiwa kumchukua, akaenda naye Dar ambapo huko baada ya kuishi kwa mwezi mmoja tu, wanaume wakaanza kumtongoza kwani ule urembo aliokuwa nao ulimvuta kila mtu aliyekuwa akimwangalia.
Uoga ulimjaa moyoni mwake, maneno aliyopewa na bi Hadija kwamba kama angefanya ujinga na wanaume hao basi angefukuzwa na kurudishwa kijijini, ukamuogopesha na hivyo kila mwanaume aliyemfuata, alimwambia kwamba hamtaki.
Ilimsaidia, aliendelea kunawiri kila siku lakini baada ya mwaka na miezi minne kukatika, mume wa bi Hadija, mzee Saidi akashindwa kuvumilia, umbo matata alilokuwa nalo Irakoze likamchanganya, kila alipokuwa akimuona, akashindwa kuvumilia, hivyo akaanza kumzengea.
Visa vikaanza, mzee Saidi akashindwa kuvumilia, umbo la msichana yule na sura yake vilimchanganya mno hivyo kuanza harakati zake ndani ya nyumba. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuomba likizo kazini, alitaka awe anabaki nyumbani na binti huyo afanye yake wakati mkewe akiwa kazini.
“Unaogopa nini Irakoze? Hebu sogea hapa kitandani,” alisema mzee Saidi, pepo la ngono lilimshika, hakutaka kuelewa kitu chochote kile, mwili wake uliwehuka, kila alipomwangalia Irakoze, alimchanganya, umbo lake, makalio yake yaliyojaajaa yalimuacha hoi, hakutaka kukubali.
“Sitaki baba, sitaki,” alisema Irakoze huku akijifanya kubisha mlangoni alipokuwa amesimama, cha ajabu, hakutaka kutoka chumbani humo.
Mzee Saidi hakutaka kulaza damu, tayari aliona kila kitu kilikuwa sawa japokuwa hakuweka usiriazi katika kumlaghai msichana huyo kuja kitandani pale alipokuwa, alichokifanya ni kusimama na kuanza kumsogelea, alipomfikia, akamshika mkono na kuanza kumvutia kwake, muda wote huo Irakoze alikuwa akiangalia chini, uso wake ulijawa na aibu mno.
“Naogopa baba,” alisema Irakoze.
“Unaogopa nini?”
“Mama atajua.”
“Atajuaje? Utamwambia?”
“Hapana!”
“Sasa atajuaje?”
Irakoze akakosa jibu, ukimya wake ulikuwa ni kama jibu lililomruhusu mzee Saidi kufanya kile alichotaka kukifanya, akamvuta, msichana huyo, akaanza kupiga hatua kuelekea kitandani, kilichofauata ni kufanya mapenzi kitandani hapo.
Huo ulikuwa mwanzo wa kudokoa asali, baada ya hapo, wakajikuta wakiingia kwenye dimbwi zito la mahaba, kila siku mzee Saidi alipokuwa akiamka, mtu wa kwanza aliyetaka kumuona alikuwa Irakoze tu.
Penzi la msichana huyo likamlevya, hakutaka kusikia chochote kile, alichokuwa akikitaka ni mapenzi motomoto tu. Hata mzee Saidi aliporudi kazini, kuna siku alikuwa akitoroka kazini na kurudi nyumbani, huko, alikuwa akifanya mapenzi na msichana huyo tu.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba kilikuwa siri kubwa, bi Hadija hakugundua chochote kile kwani maigizo waliyoyafanya wawili hao yalimpigwa upofu mkubwa, hakujua kama nyuma ya pazia alikuwa akiibiwa.
“Lakini nilikwambia simuni mke wangu!” alisema mzee Saidi, alikuwa kilalamika.
“Najua mume wangu, ila nikasahau kabisa kumwambia Irakoze kama ulikuwa ukihitaji upikiwe samaki,” alisema bi Hadija.
“Aiseee! Sasa hapa kuna umuhimu wa huyu msichana kumnunulia simu, vinginevyo kuna siku tunaweza kugombana kitu ambacho sitaki kitokee,” alisema mzee Saidi.
Hiyo ndiyo ilikuwa mbinu aliyoitumia, alitaka kuwasiliana na Irakoze kwa karibu mno, kitendo cha kurudi nyumbani ghaflaghafla kingemfanya siku kukutana na mke wake nyumbani hapo hivyo kufumwa, alichokitaka ni kuwasiliana na msichana huyo tu.
Bi Hadija hakujua, kwa fedha zake, akanunua simu na kumpa Irakoze pasipo kujua kwamba ndiyo kwanza aliliua pendo lake kwa mume wake. Hiyo ikawa nafasi nzuri kwa mwanaume huyo kuwasiliana na Irakoze ambapo kama bi Hadija hakuwepo nyumbani, walikumbatiana, walibusaiana na kupetiana kama kawaida yao.
“Siku mama akijua!”
“Unahisi atafanyaje?”
“Atanifukuza.”
“Hawezi! Mimi ndiye kidume humu ndani!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Hebu sogea kwanza unibusu hapa,” alisema mzee Saidi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimpenda kama mume wake, alimwamini sana kwani katika miaka yao kumi na tano ya ndoa hakuwahi kusikia hata siku moja akitoka nje ya ndoa yao. Alimthamini na kujiona amepata mume wa ukweli, mume aliyejua kulea na kupenda.
Siku ya kwanza aliposikia tetesi kwamba kulikuwa na uwezekano wa mume wake kutembea na mfanyakazi wake, alibisha sana na kuona kwamba watu walitaka kuivunja ndoa yao iliyodumu kwa kipindi kirefu.
Masikio akayaziba pamba, hakutaka kusikia chochote kile kutoka nje. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, tetesi zile zilizidi kuvuma kiasi kwamba akahitaji kuhakikishakwa macho yake, hakutaka kusikia tena hivyo kuanza mishemishe kwa kuwaweka walinzi ili siku mume wake akitoroka kazini, apigiwe simu.
“Nitakupigia tu shosti wangu! Mimi tena nishindwe! Hata ukitaka nivae dela wakati wa kwenda kufumania, nipo radhi na kikundi changu cha msuto,” alisema mwanamke ambaye kila siku alikuwa akimsisitizia kwamba alikuwa akichangia mapenzi yake na msichana wake wa kazi.
Siku zikaendelea kukatika, ilikuwa ni kama watu hao wamejua vile, mzee Saidi hakuwa akirudi nyumbani. Wanawake wa mtaani walizidi kusubiri lakini mzee huyo alisitisha zoezi lake la kutoroka kazini na hivyo kutulia hukohuko.
Baada ya mwezi mmoja kupita, mzee Saidi akaonekana akianza kuelekea nyumbani kwake, kama kawaida yake gari lake alilipaki mbali na nyumbani hapo ili hata mkewe akirudi, asiweze kujua kama alikuwa ndani.
“Shoga! Amekuja. Njoo haraka,” aliongea mwanamke huyo, alikuwa akimwambia bi Hadija simuni.
Wala hazikupita dakika nyingi, bi Hadija akafika mahali hapo. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili ulimtetemeka kwa hasira, alichokuwa ameambiwa, kilimtia hasira mno, akajikuta akiwa na presha kubwa ya kuingia ndani kwa lengo la kufumania.
“Subiri kwanza,” alisema mwanamke huyo, tayari wanawake wenzake walikwishakusanyika mahali hapo.
“Nina presha, niacheni niende.”
“Usiwe na presha. Ngoja kwanza tuvae madela yetu,” alisema mwanamke huyo huku wanawake waliokuwa mahali hapo wakienda makwao na kuanza kuvaa madela tayari kwa kufumania.
Wakati mambo yote hayo yakiendelea, kama kawaida, ndani ya nyumba, Irakoze na mzee Saidi walikuwa chumbani kama walivyozaliwa, walikuwa wakipeana mapenzi motomoto pasipo kujua kwamba wakati mzee huyo akiingia ndani na kupokelewa kwa mabusu mfululizo, walisahau hata kufunga mlango.
Wanawake hao wakaingia ndani na kuanza kuelekea chumbani. Mwendo wao ulikuwa ni wa kunyata huku bi Hadija akiwa na hasira mno.


ITAENDELEA...